KWA MAWASILIANO ZAIDI TUMIA BARUA PEPE rockersports212@yahoo.com AU TUPIGIE KUPITIA NAMBARI 0767166607 AU 0717166607. KARIBU SANA. 66666666607 AU 0717166607

Sunday, August 17, 2014

MUDA WA USAJILI WAONGEZWA KWA SIKU KUMI KISA LINKI YA TMS KUTOKA CAF


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeongeza kwa siku kumi muda wa kumalizika usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL)  kutokana na kuchelewa kwa link ya mfumo mpya wa usajili (system) kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Kwa mujibu wa CAF, link hiyo itakuwa tayari kwa matumizi ndani ya siku tatu zijazo kutoka sasa. 

Taarifa ya msemaji wa TFF Bonface Wambura imewataka mameneja wa usajili wa timu hizo kwa sasa kukamilisha nyaraka zote zinazotakiwa ili link hiyo itakapokuwa tayari waweze kuingiza usajili wao mara moja.

Kuanzia msimu wa 2014/2015 mfumo unaotumika kwa usajili kwa klabu hizo ni wa elektroniki badala ya ule wa zamani wa kutumia fomu za kawaida. Mfumo huo wa kisasa ambao pia unatumiwa na CAF unaondoa upungufu uliokuwepo katika mfumo wa zamani.

Kutokana na mabadiliko hayo, usajili sasa utamalizika Agosti 27 mwaka huu badala ya leo (Agosti 17 mwaka huu). Kipindi cha pingamizi ni kuanzia Agosti 28 mwaka huu hadi Septemba 3 mwaka huu.

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji itakutana kati ya Septemba 6 na 8 mwaka huu kwa ajili ya kupitia pingamizi na kuthibitisha usajili.

Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoshirikisha timu 14 itaanza Septemba 20 mwaka huu wakati ratiba inatarajia kutoka mwezi mmoja kabla ya kuanza ligi hiyo. Ligi Daraja la Kwanza inatarajia kuanza wiki ya kwanza ya Oktoba.

Mwisho wa kuombewa Hati ya Uhamisho ya Kimataifa (ITC) kwa wachezaji wanatoka nje ya Tanzania ni Septemba 6 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment