Ligi ya Mabingwa UIaya inatarajia kushuhudia sarakasi za kila aina wiki
hii, wakati awamu ya mechi za makundi ikifikia kikomo. Nafasi nane
katika awamu ya timu 16 za mwisho bado ziko wazi. Ni nani atakayefuzu?
Macho yote yanaangaziwa kundi F ambapo Napoli, Borussia Dortmund na
Arsenal zinawania nafasi mbili. Huku Juventus na AC Milan kila mmoja
akihitaji pointi moja ili kufuzu, dhidi ya wapinzani wagumu, huenda
Italia ikawa na timu zake zote tatu katika awamu ya mchujo, au iambulie
patupu kabisa. Nafasi za Benfica kufika fainali katika uwanja wao
wenyewe wa Estadio da Luz haziko mikononi mwao tena, na zitakwisha
kabisa kama Olimpiakos itawashinda Anderlecht, wakati wenzao Porto pia
wakikabiliwa na mlima mkubwa.
Chelsea tayari wamefuzu lakini watalenga kuwapiku Staeua Bucharest
Mabingwa wa Uswisi Basel, wanahitaji pointi tu ili kuendelea
mbele, kama Schalke watashindwa. Shakhtar Donetsk, Bayer Leverkusen,
Zenit St Petersburg na Ajax Amsterdam pia zina nafasi ya kufuzu.
Manchester United, Real Madrid, Paris St Germain, Bayern Munich,
Manchester City, Chelsea, Atletico Madrid na Barcelona tayari zilifuzu.
Hivyo basi mambo yatakuwa hivi:
Arsenal (pointi 12) wanasafiri kucheza ugenini dhidi ya Napoli (9)
wakihitaji sare, au kichapo kisichozidi magoli matatu, wakati Borussia
Dortmund (9), wakiweza kufuzu kama watawashinda Olympique Marseille,bila
kuzingatia matokeo mengine.
Kama Napoli na Dortmund zote zitashinda michuano yao, zitamaliza na
pointi 12 sawa na Arsenal na hivyo uamuzi wa ni nani atakayefuzu
utatokana na matokeo baina ya timu hizo tatu.
Kundi E pia litakuwa na sarakasi za aina yake, wakati Basel
(pointi 8) watakamenyana na Schalke (7) wakihitaji pointi moja tu
kujiunga na Chelsea katika awamu ya mchujo. AC Milan (pointi 8) lazima
wapate pointi wanayohitaji dhidi ya Ajax Amsterdam (7) ili kujiunga na
Barcelona kutoka kundi H.
Viongozi wa Serie A Juventus (6) watachuana na Glatasaray wakihitaji
pointi moja katika kundi B, wakati Zenit St Petersburg (6) wakipigiwa
upatu kuwafuata Atletico Madrid kutoka kundi G, wakati watakapomenyana
na Austria Vienna katika mpambano wao wa mwisho.
Porto (pointi 5) wana safari ngumu dhidi ya Atletico, wakati Benfica na
Olympiakos (zote na pointi 7) zikipambana kwa nafasi ya pili katika
kundi C ambako Paris St Germain tayari wamefuzu. Olympiakos watakabana
koo na Anderlecht huku Benfica wakiangushana na PSG.
Katika kundi A, ambapo Manchester United tayari wamefuzu, itakuwa na
sarakasi za aina yake pia. Shaktar Donetsk (8) wako katika nafasi ya
pili, lakini lazima wacheze Old Trafford huku Bayer Leverkzsen, ambao
wana pointi moja nyuma, wakisafiri kuchuana na Real Sociedad ambao wana
pointi moja pekee. Bayern Munich na Manchester City zitapimana nguvu tu
kwa sababu timu zote tayari zimefuzu katika kundi D.

No comments:
Post a Comment