KWA MAWASILIANO ZAIDI TUMIA BARUA PEPE rockersports212@yahoo.com AU TUPIGIE KUPITIA NAMBARI 0767166607 AU 0717166607. KARIBU SANA. 66666666607 AU 0717166607

Wednesday, October 17, 2012

THE ROCK CITY MARATHON NCHI NCHI TISA KUSHIRIKI

JUMLA ya nchi tisa zinatarajiwa kushiriki katika mbio za kilomita 21 za Rock City Marathon 2012, zilizoandaliwa na Kampuni ya Capital Plus International (CPI), zitakazofanyika Jumamosi Oktoba 28 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam leo, Mratibu wa mbio hizo Grace Sanga wa CPI, alizitaja nchi hizo kuwa Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC), Australia, India, Canada na Marekani, huku akidokeza maandalizi mazuri yamechangia ongezeo la washiriki.
“Tumetuma mialiko ya kushiriki kwa wadau wote wa riadha wa nchi jirani ili wapate kushiriki Rock City Marathon 2012, ndio maana tunategemea kupata washiriki wengi zaidi kutoka nje ya nchi, kulinganisha na mwaka uliopita na maboresho ya mbio hizi yatachangia kuongeza ushindani,” alisema Grace.
Sanga aliongeza kuwa, mbio hizo za kila mwaka zimegawanywa katika makundi matano ya mbio za kilomita 21 kwa wanawake na wanaume, kilomita tano kwa watu wote, kilomita tatu kwa walemavu, kilomita tatu kwa wazee kuanzia miaka 55 na kilomita mbili kwa watoto wa kati ya miaka saba hadi kumi.
Rock City Marathon zilianzishwa mwaka 2009, ambapo mwaka huu ziko chini ya udhamini wa NSSF, Airtel Tanzania, Geita Gold Mine, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), PPF, African Barrick Gold, New Africa Hotel, Nyanza Bottles, New Mwanza Hotel, TANAPA na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).
Mbio hizo zinazosubiriwa kwa hamu na wakazi wa Kanda ya Ziwa, zitapambwa na burudani ya aina yake kutoka kwa nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini Juma Kassim ‘Sir Nature’, ambapo zitaanzia kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kupitia njia tofauti na kurudi uwanjani hapo.
Aidha, Sanga alisema kuwa, pesa itakayopatikana kutokana na ada ya usajili wa washiriki unaofanyika kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza, Ofisi za Capital Plus zilizopo jengo la ATC ghorofa ya tatu na kwenye blog ya rockcitymarathon.blogspot.com zitapelekwa katika mfuko wa msaada kwa watu wenye ulemavu waishio jijini Mwanza.

No comments:

Post a Comment