Arsenal imeendelea kufanya vizuri katika michuano ya kombe
la klabu bingwa ya Ulaya baada ya ushindi wake dhidi ya Napoli ya Italy
katika uwanja wa Emirates usiku wa jana.
Nyota wa pambano hilo Mesut Ozil alifunga bao
lake la kwanza kwa Arsenal na kisha kutoa msaada wa goli la pili lililofungwa na
Olivier Giroud na kuamua hatima ya mechi hiyo katika dakika 15 za
kwanza.
Arsenal walidhibiti mchezo huo
wakionyesha ujasiri uliowawezesha kuongoza Ligi ya Premier. Ozil ambae
alisainiwa kutoka Real Madrid ndie aliyekua kichocheo kikubwa cha
Arsenal ambayo sasa inaongoza kundi la F.
Katika mechi nyingine ya kundi hilo Borussia Dortmund ya Ujerumani iliilaza Marseille ya Ufaransa kwa mabao 3-0.
Aaron Ramsey nae pia alisifiwa kwa mchezo wake
kwa kuchangia katika bao la Ozil na wachezaji hao wawili walionekana
kuonana vizuri katika safu ya viungo vya Arsenal.
Katika michuano mingine Barcelona ya Hispania
ikimkosa mchawi wao Lionel Messi ilitolewa kijasho na Celtic ya Scotland
kabla kuibuka mshindi wa 1-0 bao liliofungwa Cesc Fabregas. Celtic
walighadhabishwa na uamuzi wa kumuonyesha kadi nyekundu nahodha wao
Scott Brown kwa kumfanyia madhambi Neymar.
Chelsea iliwapa afuweni mashabiki wake kwa kuicharaza Steaua Bucharest ya Rumania kwa mabao 4-0.
Athletico Madrid ya Hispania iliilaza Porto ya
Ureno 2-0 na Mario Balotelli aliiokoa AC Milan ya Italy kwa bao la
penalti katika kipindi cha majeruhi na kutoka sare 1-1 na Ajax ya
Uholanzi .
No comments:
Post a Comment