Wachezaji Mbwana Samata na Thomas
Ulimwengu wametua Dar es Salaam leo (Mei 17 mwaka huu) mchana, na kujiunga moja
kwa moja kwenye kambi ya Taifa Stars kwa ajili ya michuano ya Afrika dhidi ya
Zimbabwe (Mighty Warriors).
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya
kwanza ya michuano hiyo itafanyika kesho (Mei 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Washambuliaji hao wa Taifa Stars wamewasili
saa 7.25 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines wakitokea Khartoum, Sudan
ambapo jana (Mei 16 mwaka huu) timu yao ya TP Mazembe ilicheza mechi ya Ligi ya
Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya huko.
Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij
amesema kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mechi hiyo, kwani kimepata mechi
za kirafiki na mazoezi ya kutosha kwenye kambi iliyoanzia Tukuyu mkoani Mbeya
ambapo kulikuwa na utulivu mkubwa.
Naye Kocha Msaidizi wa Zimbabwe, Kalisto
Pasuwa amesema hawaifahamu vizuri Taifa Stars lakini wamekuja kwenye mechi hiyo
itakayoanza saa 10 jioni kwa ajili ya kushinda, na kuwataka washabiki
wajitokeze kwa wingi kuona kiwango cha timu yake.
Milango kwa ajili ya mechi hiyo
itakayochezeshwa na waamuzi kutoka Ghana wakiongozwa na Joseph Odartei Lamptey
itakuwa wazi kuanzia saa 6 kamili mchana, na tiketi zitapatikana katika magari
maalumu uwanjani hapo.
Viingilio katika mechi hiyo ni sh.
5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, kijani na bluu, sh. 10,000 kwa VIP C na B,
na sh. 20,000 kwa VIP A.
No comments:
Post a Comment