Upangaji
ratiba (draw) ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) uliokuwa ufanyike juzi
(Mei 3 mwaka huu), sasa utafanyika Jumanne (Mei 7 mwaka huu) na ligi
hiyo itaanza Mei 12 mwaka huu kama ilivyopangwa.
Uamuzi
huo umefanya na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) iliyokutana leo (Mei 5 mwaka huu) kujadili maandalizi ya
ligi hiyo, yakiwemo maombi ya baadhi ya mikoa ambayo haijamaliza yao
kutaka RCL isogezwe mbele.
Kamati
ya Mashindano chini ya Uenyekiti wa Blassy Kiondo ambaye pia ni mjumbe
wa Kamati ya Utendaji ya TFF ilipitia maombi hayo na kuangalia athari
ambazo zinaweza kujitokeza huko mbele iwapo RCL itasogezwa mbele.
Baadhi
ya athari iwapo RCL itasogezwa mbele ni timu zitakazopanda daraja
kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kutopata muda wa kufanya usajili wa
wachezaji kwa msimu mpya.
Hivyo
draw hiyo itakayofanyika saa 6 mchana itahusisha mikoa ambayo tayari
imemaliza ligi na kuwasilisha majina ya mabingwa wao. Mabingwa ambao
wamewasilishwa na mikoa yao kwenye mabano ni Abajalo SC (Dar es Salaam
2), Biharamulo FC (Kagera), Flamingo SC (Arusha), Friends Rangers (Dar
es Salaam 3), Katavi Warriors (Katavi), Kiluvya United (Pwani), Kimondo
FC (Mbeya) na Machava FC (Kilimanjaro).
Mingine
ni Magic Pressure FC (Singida), Mbinga United (Ruvuma), Mji Njombe
(Njombe), Polisi Jamii Bunda FC (Mara), Red Coast FC (Dar es Salaam 1),
Rukwa United (Rukwa), Saigon FC (Kigoma), TECKFOLT FC ya Kilombero
ambayo ni Shule ya Sekondari (Morogoro) na UDC FC ya Ukerewe (Mwanza).
Ada
ya ushiriki ni sh. 100,000 wakati usajili wa wachezaji wa timu hizo ni
uleule uliofanyika katika Ligi ya Mkoa na unatakiwa kuwasilishwa TFF kwa
ajili ya uthibitisho. TFF inapenda kusisitiza kuwa hakuna usajili mpya
wa wachezaji kwa ajili ya ligi hiyo.
Mikoa
iliyoshindwa kuwasilisha mabingwa wake ni Dodoma, Geita, Iringa, Lindi,
Manyara, Mtwara, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Tanga.
No comments:
Post a Comment