Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete jana amezindua ujenzi wa kituo cha vijana cha michezo cha kimataifa mjini Dar es Salaam.
Mwandishi
wa BBC Baruan Muhuza aliyehudhuria shughuli hiyo amesema kuwa mradi huo
unagharamiwa kwa pamoja na kampuni ya nishati ya umeme Symbion Power ya
Marekani na klabu ya soka ya Sunderland inayoshiriki ligi kuu ya
England.
Katika sherehe za uzinduzi huo kwenye eneo la Kidongo
Chekundu Mnazi Mmoja Rais huyo aliungana kwa pamoja na Afisa Mtendaji
Mkuu wa Sunderland Margaret Bryne na Afisa Mtendaji Mkuu wa Symbion
Power Paul Hinks.
Akizungumza katika shughuli hiyo Bryne alisema “Tunafurahia kuwa hapa Tanzania leo na kuona maendeleo yanayofanywa na mradi huu.
Uwanja
huu wa michezo ni sehemu ya msingi wa ushirikiano wa kipekee kati yetu
na kandanda ya Tanzania, ni furaha kuona kituo hiki kikijengwa.”
Kituo
hicho kitakapokamilika mwezi machi 2015 kitakuwa na uwanja mkubwa wa
soka wenye nyasi za bandia za kiwango cha kimataifa cha 3G, uwanja wa
wachezaji watano kila upande, viwanja viwili vya mchanga na uwanja wa
mpira wa kikapu na wavu.
Katika mradi huu kampuni ya Symbion Power
inagharamia ujenzi wa kila kitu katika kituo hicho huku Klabu ya
Sunderland ikitoa wataalamu wa ufundi na mafunzo ya soka kwa watoto na
vijana.
Akihutubia umma wa watu waliojitokeza katika shughuli ya
uzinduzi huo, Rais Kikwete alieleza matumaini yake ya matunda
yatakayotokana na mradi huo, huku akielezea jinsi alivyopata wazo la
kuanzishwa kwa kituo hicho ambacho kimepewa jina lake.
No comments:
Post a Comment