Augsburg walijizatiti ili kuwazaba Mainz mabao mawili kwa moja ikiwa ni
ushindi wao wa kwanza msimu huu katika mechi sita.
Nayo Bayer Leverkusen
iliduwazwa na Eintracht Braunschweig.
Kocha wa Augsburg Markus Weinzierl alisema baada ya mechi "Kama tu
ilivyo katika kila mechi, tulipigana kweli kweli na kupata nafasi.
Nadhani hicho kinaonyesha tofauti yetu na pia hatukukata tamaa.
Tulicheza mechi tano bila kushinda lakini tulikuwa na ari nzuri katika
timu. Nadhani tunaweza kujivunia."
Andre Hahn alitikisa wavu mara mbili wakati Augsburg ikipanda kutoka
eneo la kushushwa daraja na kutoshana na Mainz kwa pointi 13. Katika
mechi nyingine ya jana, Sergio Garcia alifunga goli katika dakika za
mwisho na kuisaidia Werder Bremen kutoka nyuma na kuwashinda Hannover
mabao matatu kwa mawili.
Ushindi huo umewaweka Bremen katika nafasi ya
nane na pointi 15, ikiwa ni mbili mbele ya Hannover ambao wamepata
pointi moja tu kutokana na mechi zao tano za mwisho.
Wachezaji wa Werder Bremen wakisheherekea ushindi wao dhidi ya Hannover 98
Thomas Eichin ni mkurugenzi mkuu wa Werder Bremen "Nilikuwa na
imani na timu, ambayo imefanya vyema.
Ulikuwa mchezo mzuri wa Bundesliga
baina ya timu mbili. Ulikuwa mchuano mzuri kuutazama na nina furaha
kuwa tumeweza kuwapa mashabiki ushindi wa nyumbani. Na sasa tunaangazia
mechi zijazo tukiwa na utulivu"
Jumamosi, Bayern Munich walitokwa jasho katika ushindi wao wa mabao
mawili kwa moja dhidi ya Hoffenheim ili kusalia kileleni mwa ligi pointi
moja mbele ya Borussia Dortmund ambao siku ya Ijumaa waliwachabanga
Stuttgart magoli sita kwa moja.
Kocha wa Hoffenheim Markus Gisdol
alikuwa na haya ya kusema baada ya mechi "kuna mchanganyiko wa hisia,
kwa sababu tulikuwa na mchezo mzuri lakini kwa bahati mbaya mwishowe
hatukupata hata pointi."
Bayer Leverkusen wanasalia katika nafasi ya tatu na tofauti ya pointi
tatu nyuma ya Dortmund baada ya kuduwazwa Jumamosi kwa kufungwa bao moja
bila jawabu na washika mkia Eintracht Braunschweig.
No comments:
Post a Comment