Ureno imeanza vizuri kuwania nafasi ya kucheza katika fainali za kombe
la dunia mwakani baada ya kuishinda Sweden kwa bao 1-0, Ufaransa
yateleza, wakati matumaini ya Ugiriki yakiongezeka kuelekea Brazil.
Alikuwa Cristiano Ronaldo maarufu kama CR7 ambaye alikuwa shujaa wa
Ureno jana usiku wakati alipopachika bao la kichwa ambalo linaiweka timu
ya taifa hilo katika nafasi nzuri ya kukata tikiti yake katika fainali
za kombe la dunia mwakani nchini Brazil, baada ya kuishinda Sweden kwa
bao 1-0.
Hili ni pigo la binafsi alilotoa Ronaldo kwa Zlatan Ibrahimovic katika
mpambano kati ya nyota hao, ambapo mmoja wao atabakia nyumbani wakati wa
tamasha la soka kule Brazil mwakani. Hadi alipopachika bao hilo,
Ronaldo alikuwa akisumbuliwa mno na ukuta mgumu wa Sweden , alipoteza
mikwaju miwili kwa kubamiza mipira katika ukuta huo wa walinzi wa Sweden
na alipewa kadi muda mfupi kabla ya bao lake kwa kumfanyia rafu mlinda
mlango wa Sweden Andreas Isaksson na fadhaa yake ilipanda zaidi.
Sweden ilipata nafasi kadha katika kipindi cha kwanza kabla ya Ureno
kuchukua udhibiti wa mchezo huo baada ya mapumziko, na kupata nafasi ya
uongozi katika mchezo wa duru ya pili utakaofanyika hapo Jumanne ijayo.
Ufaransa yageuka kichwa cha mwendawazimu
Wakati Ureno ikijiwinda kuelekea Brazil mwakani.
Kigogo cha soka barani
Ulaya Ufaransa kiko katika hatari ya kuwa mtazamaji , baada ya
kuadhiriwa na Ukraine kwa kufungwa mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza
hapo jana . Iceland ikiwa na wachezaji 10 uwanjani ilipambana na
kufanikiwa kutoka sare ya bila kufungana dhidi ya Croatia mjini
Reykjavic na kuweka matumaini yake hai ya kuweza kufuzu kucheza katika
fainali muhimu za kimataifa kwa mara ya kwanza , wakati Ugiriki ikitoka
kifua mbele dhidi ya Romania kwa kuichapa mabao 3-1 mjini Athens.
Miongoni mwa timu nane za bara la Ulaya ambazo zinawania fursa ya mwisho
baada ya kushindwa kupata tikiti ya moja kwa moja kuelekea Brazil ,
Ufaransa iko katika hali mbaya zaidi wakati wakiingia katika mchezo wa
mwisho wiki ijayo baada ya usiku mbaya kabisa mjini Kiev jana.
Magoli ya kipindi cha pili yaliyowekwa wavuni na Roman Zozulia na Andriy
Yarmolenko pamoja na kadi nyekundu dhidi ya mlinzi wa Ufaransa Laurent
Koscielny yalifanya kuwa usiku wa kustahili kusahaulika kwa kikosi hicho
cha kocha Didier Deschamps , ambacho kinahitaji uhai wa kutosha mjini
Paris siku ya Jumanne ili kufanyia ukarabati madhara hayo yaliyotokea.
Lakini kocha Didier Deschamps amesema kuwa kikosi chake kina nafasi ya
kufuzu katika mchezo wa mwisho hapo Jumanne , licha ya kukiri kuwa
kikosi chake kilishindwa kuhimili vishindo vya wapinzani wao Ukraine na
kukubali kipigo hicho cha mabao 2-0.
Mbali ya michuano hiyo ya kuwania kufuzu kucheza katika fainali za kombe
la dunia mwakani, lakini pia kulikuwa na mapambano ya kirafiki katika
bara la Ulaya na kwingineko. Italia timu inayoipa Ujerumani ndoto za
jinamizi kila mara imethibitisha kuwa haina nafasi ya kuiachia Ujerumani
kutamba mahali popote baada ya jana kutoka sare ya bao 1-1 katika
mchezo wa kirafiki mjini Milan.
Ujerumani ilishindwa kufurukuta dhidi ya
mahasimu wao hao jana katika mchezo ambapo kocha Joachim Loew
alisherehekea mchezo wake wa 100 tangu kuchukua uongozi wa kikosi hicho.
Chile mwiba kwa Uingereza.
Uingereza ambayo inacheza na Ujerumani katika mchezo mwingine wa
kirafiki wiki ijayo, ilijikuta ikisalimu amri mbele ya Chile ambayo
ilikuwa mwiba mbele ya vigogo hao wa soka katika bara la Ulaya.
Kocha wa
Uingereza Roy Hodgson ameapa kuwa atarejesha kikosi chake cha kwanza
kwa ajili ya mchezo wa Jumanne dhidi ya Ujerumani baada ya kukiona
kikosi chake kisicho na uzoefu kikipokea kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya
Chile.
Michezo mingine ya kirafiki ilikuwa ni baina ya Korea ya kusini dhidi ya Uswiz, ambapo Korea Kusini ilichapa Uswisi kwa
mabao 2-1, Urusi ikatoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Serbia, Jamhuri ya
Ireland ikaichapa Latvia kwa mabao 3-0.
Swaziland ilikubali kipigo cha
mabao 3-0 dhidi ya Afrika kusini na Belarus ikatoka sare ya bila
kufungana na Albania.
Barani Afrika, Mabingwa wa Afrika Nigeria wanatarajiwa
kujihakikishia nafasi yao katika kombe la Dunia mwakani ,
lakini Cameroon na Cote d'Ivoire wanakabiliwa na mtihani mkubwa dhidi ya
Tunisia na Senegal.
Nigeria wanacheza leo Jumamosi katika mchezo wa mkondo wa pili dhidi ya Ethiopia wakiwa na faida ya magoli mawili kwa
moja kutokana na mechi ya mkondo wa kwanza iliyochezwa mjini Addis
Ababa.
Cameroon na Tunisia zilitoka sare ya kutofungana bao mjini Tunis,
nayo Cote d'Ivoire ikaizaba Senegal tatu kwa moja nyumbani.
No comments:
Post a Comment