Timu ya
Taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes)
imeahidi ushindi kwenye mechi yake dhidi ya Nigeria (Flying Eagles)
itakayochezwa kesho (Julai 29 mwaka huu).
Mechi hiyo
ya kwanza ya raundi ya pili kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Afrika kwa
vijana wenye umri huo zitakazofanyika mwakani nchini Algeria itachezwa kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Akizungumza
kwenye mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika leo (Julai 28 mwaka huu)
ofisi za TFF, Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes, Jakob Michelsen na nahodha wake
Omega Seme wamesema timu yao iko tayari kwa mechi hiyo itakayochezeshwa na
waamuzi kutoka Kenya.
Michelsen
amesema timu yake imepata mechi mbili za kujipima nguvu dhidi ya Rwanda, lakini
pia aliishuhudia Flying Eagles ikicheza mechi ya kirafiki na Rwanda (Young
Amavubi) uliofanyika Julai 24 mwaka huu jijini Kigali.
“Timu iko vizuri na wachezaji kama Frank
Domayo, Simon Msuva na Ramadhan Singano ambao pia wanachezea timu A (Taifa
Stars), hivyo uzoefu wao ni muhimu kwa mechi ya kesho.
“Nigeria ni mabingwa watetezi wa michuano hii
kwa hiyo tunatarajia upinzani mkubwa, lakini tumejiandaa kwa hilo. Nigeria ni
nchi yenye mfumo mzuri wa timu za vijana, na sisi tunaelekea huko huko” amesema
Michelsen.
Naye Kocha
Mkuu wa Flying Eagles, John Obuh amesema haijui vizuri Ngorongoro Heroes lakini
anaiheshimu kutokana na ukweli kuwa inacheza raundi ya pili baada ya kuitoa
Sudan katika raundi ya kwanza.
“Sina mchezaji yeyote anayecheza mpira wa
kulipwa nje ya Nigeria, lakini tumekuja kushinda ili kujiweka katika nafasi
nzuri ya kucheza raundi ya mwisho na hatimaye tucheze fainali mwakani,” amesema
Obuh aliyefuatana na nahodha wake Samuel Okan ambaye ni mlinda mlango.
Viingilio
katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Moses Osano ni sh. 3,000 kwa viti
vya rangi ya chungwa, bluu na kijani wakati VIP B na C itakuwa sh. 5,000.
Kiingilio kwa VIP A ni sh. 10,000.
Osano
atasaidiwa na Peter Keireini na Elias Wamalwa wakati mwamuzi wa mezani (fourth
official) ni Thomas Onyango. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Charles Masembe
kutoka Uganda.


No comments:
Post a Comment