Shirikisho la sika nchini Tanzania TFF limepokea barua kutoka shirikisho la soka duniani FIFA likiarifu kuwa kocha wa zamani wa mabingwa wa soka Afrika mashariki na kati Yanga Costadian Papic, amewasilisha mashitaka yake ndani ya FIFA juu ya Yanga kuendelea kutokumlipa malimbikizo ya mshahara wake wakati akiifundisha timu hiyo.
Papic anaidai Yanga kiasi cha Dolari za kimarekani milioni 12.3, ambapo FIFA imemtaka mwanachama wake TFF kuijulisha Yanga juu ya hilo.
Lakini wakati hilo likiendelea TFF imelikumbusha deni lingine la mchezaji wa zamani wa Yanga John Njoroge deni ambalo mpaka sasa halijalipwa na Yanga, klabu kongwe nchini na barani Afrika kwa ujumla.
Akiongea na waandishi wa habari katibu wa TFF Angetile Oseah amesema TFF imetoa muda kwa Yanga kulipa deni hilo na endapo watashindwa kufanya hivyo ndani ya muda huo basi moja kati ya mambo mawili yatafanyika ambayo ni ama Yanga kushushwa daraja au kupokwa points zake za ligi.
Oseah ameitaka Yanga kufanya hivyo mapema kwani kwa hali ilivyo sasa ni kwamba wanaendelea kulipaka matope soka la nchi hii na Taifa kwa ujumla.
Sambamba na hilo TFF imesikitishwa na kitendo cha uongozi wa Yanga kuwatimua kazi watendaji wake wote wa kuajiriwa kwa maana ya sekretarieti nzima.
Akitoa masikitiko hayo katibu wa TFF Oseah amesema kitendo hicho si tu kimeonyesha wazi ni namna gani uongozi wa Yanga ulivyokuwa mbali na matatizo ya klabu yao bali pia kimeendelea kupoteza rasilimali watu muhimu ambao tayari walikwisha kupata mafunzo na semina mbalimbali za kiutendaji katika soka.
Oseah amesema pamoja na uongozi wa Yanga kuchukua maamuzi hayo kwa watendaji wao, TFF bado hawajapata taarifa rasmi ya kuondolewa kwa watendaji hao wa zamani wa Yanga mbali na kuzisikia kupitia vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na TFF kuendelea kumtambua kocha wa Yanga kuwa ni Thom Seintfiet ambaye naye alitimuliwa.
No comments:
Post a Comment