Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya
(FKF) wamefikia makubaliano ya kushirikiana katika maeneo mbalimbali kwa
lengo la kuinua kiwango cha mpira wa miguu katika nchi hizo.
Akizungumza
baada ya mkutano uliowakutanisha vinara wa mashirikisho hayo Dar es
Salaam jana, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema wameamua kurejesha
uhusiano huo uliokuwepo zamani baada ya kuwepo utulivu katika uendeshaji
mpira wa miguu nchini Kenya.
Amesema
maeneo ya ushirikiano ambayo wameagiza yafanyiwe kazi na sekretarieti
za pande zote (TFF na KFF) ili baadaye yaingizwe katika Hati ya
Makubaliano (MoU) ni mafunzo, waamuzi, mechi za timu za Taifa za
wakubwa, vijana na wanawake, na Ligi Kuu.
Rais
Tenga pia amesema wameamua kuwepo ziara za mafunzo (study tours) katika
maeneo mbalimbali ambapo kwa Kenya wao Ligi Kuu yao iliingia katika
mfumo wa kampuni mapema, hivyo itakuwa fursa nzuri kwa Bodi ya Ligi Kuu
ambayo iko kwenye mchakato wa kuanzishwa kupata uzoefu kwa wenzao wa
Kenya.
Naye
Rais wa FKF, Sam Nyamweya aliyefuatana na Makamu wake wa Rais, Robert
Asembo amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya ni wa kihistoria,
hivyo wameamua kuuanzisha upya kwa faida ya nchi hizo.
Amesema
hivi karibuni FKF ilichukua waamuzi kutoka Tanzania waliochezesha mechi
ya kirafiki kati ya Kenya (Harambee Stars) na Afrika Kusini (Bafana
Bafana), hivyo wameamua kubadilishana waamuzi kwa lengo la kuwaongezea
uzoefu.
“Waamuzi
wa Tanzania walichezesha vizuri mechi ile. Unajua kwetu kuna upinzani
mkubwa katika klabu kama AFC Leopards na Gor Mahia, ukipanga refa
utasikia wengine wanalalamika, mara huyo ni Mjaluo. Hata akichezesha
vizuri bado watalalamika tu kutokana na upinzani uliopo katika klabu
hizo,” amesema.
Rais
Nyamweya ameongeza kuwa ili kuondoa malalamiko katika mechi za aina
hiyo wanaweza kuchukua waamuzi kutoka Tanzania, na vilevile waamuzi
kutoka Kenya wakachezesha mechi za aina hiyo nchini Tanzania.
Amesema
vilevile wamepanga kuangalia uwezekano wa kuwa na mechi za kuandaa timu
kabla ya kuanza Ligi Kuu za nchi hizo ambapo washindi watatu au wanne
wa kwanza katika ligi hizo kushindana.
Kwa
upande wa mafunzo, wamekubaliana kuwa kwa vile kila nchi ina wakufunzi
wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na la
Afrika (CAF) watawatumia kuandaa mafunzo ya mara kwa mara kwa waamuzi,
makocha, madaktari wa tiba ya michezo na viongozi badala ya kusubiri
mafunzo ya aina hiyo kutoka kwa mashirikisho hayo ya kimataifa.
No comments:
Post a Comment