Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) ilianza tarehe 12 Mei 2013
ikishirikisha klabu bingwa za mikoa yote ya Tanzania Bara, isipokuwa
mikoa ya Pwani na Manyara ambayo kutokana na sababu tofauti ilishindwa
kuwasilisha majina ya klabu zake hadi siku ya mwisho iliyowekwa na
Kamati ya Mashindano, yaani tarehe 10 Mei 2013.
Suala
la kukosekana kwa wawakilishi wa mikoa hiyo miwili limezua maswali
mengi kiasi kwamba Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
linalazimika kutoa ufafanuzi kwa faida ya wadau wote wa mpira wa miguu.
Ligi
ya Mabingwa wa Mikoa, ambayo ni mpya baada ya TFF kubadilisha mfumo wa
uendeshaji wa mpira wa miguu, ilipangwa kuanza tarehe 5 Mei 2013, lakini hadi tarehe ya mwisho ya kuwasilisha majina ya mabingwa wa mikoa, yaani tarehe 2 Mei 2013 mikoa michache ndiyo iliyokuwa imemaliza ligi zao na kupata mabingwa.
Kuchelewa
huko kwa mikoa kumaliza ligi zao kuliilazimisha Kamati ya Mashindano ya
TFF kuongeza muda wa mikoa kuwasilisha majina ya wawakilishi hao hadi
tarehe 10 Mei 2013 na hivyo siku ya kuanza kwa Ligi kusogezwa mbele hadi
tarehe 12 Mei 2013.
Hadi
kufikia tarehe hiyo mpya ya mwisho ya kuwasilisha majina ya mabingwa wa
mikoa, ni mikoa sita tu iliyofaidika na kuongezwa huko kwa muda na
kupata wawakilishi wake. Mikoa hiyo ni Iringa, ambayo pamoja na
kuongezwa kwa muda, iliandika barua ya kuihakikishia Kamati ya
Mashindano kuwa itapata bingwa kabla ya kuisha kwa siku ya tarehe 10 Mei
2013.
Mikoa mingine ni Lindi, Mtwara, Geita, Tabora na Dodoma.
Mkoa
wa Manyara haukuweza kumaliza ligi yake hadi mwisho wa siku ya tarehe
10 Mei 2013 na hivyo Kamati ya Mashindano iliyosubiri majina hadi saa
12:00 jioni siku hiyo kuamua kuwaondoa wawakilishi wa Manyara kwenye
ratiba.
Awali, Kamati ya Mashindano iliamua kuwa ratiba ya mechi za Ligi ya Mabingwa wa Mikoa ipangwe tarehe 7 Mei 2013,
ikishirikisha mikoa ambayo ilishapata mabingwa wake, lakini baada ya
kuona baadhi ya mikoa ilikuwa haijakamilisha ligi zake, Kamati iliamua
kuwa ratiba ipangwe kwa kutumia majina ya mikoa kwa matumaini kuwa hadi
kufikia tarehe 10 Mei 2013, mikoa itakuwa imeshapata wawakilishi wake na
kwa kuwa ratiba inahusu mikoa jirani, ingekuwa rahisi kwa timu kusafiri
kutoka kituo kimoja hadi kingine.
Lakini
Mkoa wa Manyara haukuweza kufanya hivyo na Kamati kulazimika kuuondoa
kwenye ratiba kutokana na kushindwa kukidhi utashi huo.
Mkoa
mwingine ambao uliondolewa kwenye ratiba ni Pwani ambayo pamoja na
kutuma jina la mwakilishi wake, Kamati ilipokea malalamiko kutoka klabu
zilizoshiriki Ligi ya Mkoa, zikidai kuwa jina la bingwa wa Pwani
lililowasilishwa TFF lilikuwa batili kwa kuwa klabu ya Kiluvia United
haikustahili kushiriki Ligi ya Mkoa kutokana na ukweli kuwa
haijasajiliwa mkoani Pwani na wala haikushiriki ligi ya mkoa msimu
uliopita. Kamati ya Mashindano iliiondoa Pwani kwenye ratiba na
kulirudisha suala hilo mkoani.
Ingawa
Katibu wa Pwani alijaribu kuishawishi Sekretarieti ya TFF iliangalie
suala hilo kwa undani zaidi, Sekretarieti ilimjibu kuwa lilishafanyiwa
uamuzi na Kamati, hivyo uamuzi huo usingeweza kutenguliwa na kumshauri
katibu huyo arejee mkoani kwake kuwasiliana na viongozi wenzake kuona ni
jinsi gani mkoa unaweza kunusuru hali hiyo kwa kufanya uamuzi ambao
ungeuwezesha mkoa kupata mwakilishi.
Kwa
mantiki hiyo, masuala ya Manyara na Pwani yalikuwa ndani ya uongozi wa
mikoa husika na si Kamati ya Mashindano ya TFF kwa kuwa Kamati ilitaka
ipatiwe jina la bingwa ambaye alipatikana kwa mujibu wa mfumo mpya wa
Ligi ya Mikoa.
Ligi
ya Mabingwa wa Mikoa inachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini na
hivyo timu zilizokutana tarehe 12 Mei 2013, zitarudiana mwishoni mwa
wiki hii na kupatikana timu zitakazosonga mbele kwenye raundi nyingine
hadi timu tatu bora zitakazopanda daraja kwenda Ligi Daraja la Kwanza
(FDL) zitakapopatikana.
Ligi
za Mikoa, kwa mujibu wa kanuni mpya, zinatakiwa ziwe na timu kati ya 16
na 20 na zinatakiwa zicheze mechi mbili za nyumbani na ugenini, hata
kama zitakuwa zinatumia uwanja mmoja.
Uamuzi
wa kubadilisha mfumo huo ulifanywa ili kuhakikisha kuwa mikoa inakuwa
na na mashindano kwa mwaka mzima na hivyo kuiwezesha mikoa kujikita
katika kutafuta mbinu za kupata fedha na kuendeleza mchezo wa mpira wa
miguu kwenye mikoa yao.
Uamuzi
huo pia unasaidia kupunguza mtindo wa wachezaji kuzunguka klabu tofauti
katika msimu mmoja kwa kuwa wanalazimika kutulia kwenye klabu moja hadi
muda wa usajili unapofika.
Pamoja
na wachezaji kutulia sehemu moja kwa muda mrefu, pia walimu wanapata
fursa ya kujikita vizuri kwenye programu zao kwa kuwa wanakuwa na uwezo
wa kufuatilia maendeleo ya wachezaji wao.
Pamoja
na hayo yote, mfumo huo utasaidia kurudisha msisimko kwenye mikoa na
hivyo kutoa fursa kwa vijana wengi wenye vipaji kuonekana na
kuendelezwa.
TFF
inatoa wito kwa viongozi wa mikoa kuanza kubuni sasa mikakati ya
kuendesha ligi hizo msimu unaokuja kwa kuwa hakutakuwa na nafasi tena ya
kuongeza muda kwa mikoa kuwasilisha majina ya wawakilishi wao.
No comments:
Post a Comment