Kocha
Mkuu wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage amesema kikosi chake kiko tayari kwa
ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Zambia
itakayochezwa keshokutwa (Ijumaa) jijini Lusaka.
Akizungumza
kwenye hafla ya kuiaga timu hiyo iliyofanyika leo (Februari 12 mwaka huu)
kwenye ofisi za TFF jijini Dar es Salaam, Kocha Kaijage amesema wachezaji wake
wako vizuri, ingawa hakuwa tayari kutoa ahadi kuhusu matokeo.
“Vijana
wako vizuri, lakini sitaki kutoa ahadi. Watanzania watuombee, watuunge mkono
ili tuweze kufanya vizuri,” amesema Kocha Kaijage katika hafla hiyo ambayo
mgeni rasmi alikuwa Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert
Bayi.
Twiga
Stars inaondoka na kikosi cha wachezaji 19 na benchi la ufundi lenye watu
watano kwa ndege ya Fastjet kwa ajili ya mechi hiyo itakayooanza saa 9 kamili
kwa saa za Zambia. Msafara wa timu hiyo unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya
Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Wachezaji
waliopo kwenye kikosi hicho chini ya nahodha Sophia Mwasikili ni Amina Ali,
Anastazia Katunzi, Asha Rashid, Donisia Minja, Esther Chabruma, Etoe Mlenzi,
Everine Sekikubo, Fatuma Issa, Fatuma Makusanya, Fatuma Mwisendi, Fatuma Omari,
Happiness Mwaipata, Maimuna Mkane, Mwapewa Mtumwa, Sherida Boniface, Therese
Yona, Vumilia Maarifa na Zena Said.
Wakati
huo huo, timu ya Azam imeondoka leo alfajiri (Februari 12 mwaka huu) kwenda
Beira, Msumbiji kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho dhidi Ferroviario
da Beira itakayochezwa Jumamosi. Msafara wa timu hiyo unaongozwa na mjumbe wa
Kamati ya Utendaji ya TFF, James Mhagama.
Naye
mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Nassib Ramadhan ataongoza msafara wa timu
ya Yanga inayoondoka kesho mchana kwenda Comoro kwa ajili ya mechi ya marudiano
ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Komorozine itakayochezwa Jumamosi.
No comments:
Post a Comment