Kocha Jürgen Klopp ametia saini ya kuurefusha mkataba wake katika klabu
ya Borussia Dortmund kwa miaka miwili zaidi hadi mwaka wa 2018.
Klabu ya
Dortmund inastahili kujivunia sana kazi anayowafanyia.
Klopp ambaye ni mmoja wa makocha wanaomezewa mate sana barani Ulaya,
alijiunga na Dortmund mwaka wa 2008, na kuwaongoza kunyakua taji la
Bundesliga mwaka wa 2011 pamoja na ligi ya nyumbani na kombe la
shirikisho katika mwaka wa 2012 kabla ya kushindwa na mahasimu wao wa
Ujerumani Bayern Munich katika fainali ya Champions League msimu huu.
Huku akianzisha enzi ya kabumbu safi la kasi na kuvutia, ambalo
limewavutia mashabiki wengi kote ulimwenguni, kuwasili kwa Klopp
kulifungua ukurasa mpya kwa mabingwa hao wa Champions League mwaka wa
1997 ambao nusra wafilisike kabisa takribani miaka kumi iliyopita.
Klopp amewaambia waandishi wa habari baada ya kusaini mkataba huo kuwa
“hakuna anayestahili kupiga simu hadi mwaka wa 2018”. Amesema wanahisi
kuwepo imani kubwa na matumaini katika klabu hiyo na hiyo ni dalili
nzuri.
Amesema ni heshima kuwa baadhi ya vilabu vikuu ulimwenguni vinaona kuwa
BVB inafanya kazi nzuri lakini yeye siyo sehemu ya wale wanaohisi kuwa
kuna lishe nzuri zaidi kwingineko.
Mikataba ya wafanyakazi wenzake
katika klabu hiyo pia imerefushwa katika juhudi za kuendeleza mafanikio
ambayo wamepata katika miaka ya karibuni.
No comments:
Post a Comment