Yayo Kato akijishauri cha kufanya kabla ya kuanza kukimbizana na Ally Hamza wa JKT Oljoro. |
Coastal Union ina mashabiki wa mataifa mengi. |
Viongozi wa Coastal Union wakifuatilia mechi ya leo uwanja wa Mkwakwani. |
Pamoja na kuweka kambi nchini Oman kwa wiki mbili, kikosi cha Coastal
Union ya Tanga kimeshindwa kuwapa raha wapenzi wake katika uwanja wa Mkwakwani mjini
Tanga baada ya kulazimishwa sare na wanajeshi wa JKT Oljoro kutoka Arusha.
Suluhu ya 1-1 imeonekana kuwavunja nguvu viongozi na
mashabiki wa Coastal Union, ambao waliingia uwanjani kwa idadi ndogo kutokana
na tatizo la ukataji tiketi kuwakwaza baadhi ya mashabiki waliotaka kuiangalia
timu yao iliyotoka Oman wiki hii.
Coastal Union walianza mchezo wa leo kwa kujiamini wakitoa
pasi za uhakika huku wakifika katika lango la wapinzani wao mara kwa mara.
Kunako dakika ya 7, Yayo Kato aliandika bao la kwanza
baada ya kupokea pasi murua kutoka kwa Kenneth Masumbuko baada ya Hamad Juma
kufanya kazi nzuri ya kumdhibiti beki wa Oljoro na kupiga krosi.
Bao hilo lilidumu kwa dakika 45 za awali ambapo mpaka timu
zinakwenda mapumziko ubao uliendelea kusomeka 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku wachezaji wa Oljoro
wakicheza kw akujihami na kupiga pasi fupi zilizoonyesha kuwachanganya
wachezaji wa Coastal Union.
Kufikia dakika ya 75 Coastal Union, tayari walishafanya
mabadiliko ya wachezaji watatu ambapo alitoka Kenneth Masumuko na kuingia Abdi
Banda, baadae alitoka Othamn Tamim akaingia Crispian Odula mwisho alitoka Yayo
Kato na kuingia Mohammed Miraji.
Wagosi wa Kaya waliendelea kumiliki mchezo na kumtumia zaidi Danny Lyanga alikuwa msumbufu katika winga ya kushoto na mara kadhaa kupiga hodi kwa mlinda mlango wa Oljoro, Mohammed Yusuf.
Ilipotimu dakika ya 87 dakika chache kabla ya mwamuzi wa leo
Israel Nkongo kumaliza kipute, Hamis Saleh wa JKT Oljoro alitumia vema makosa
ya mabeki wa Coastal Union na kupachika bao lililoamsha benchi la timu yake kwa
furaha.
Dakika ya 89 Crispian Odula alipata pasi akiwa ndani ya 18
lakini akapiga shuti hafifu lililotua ndani ya mikono ya golikipa wa Oljoro.
Mpaka mchezo unakamilika, ubao ulisomeka 1-1 hali iliyowatoa
kichwa chini wachezaji na mashabiki wa Wagosi wa Kaya waliokuwa na matumaini
makubwa ya kushinda.
No comments:
Post a Comment