Wakati huo huo kesho Jumanne inaanza michezo ya robo fainali ya kombe la
shirikisho la Ujerumani DFB Pokal , ambapo Eintracht Frankfurt
inaikaribisha nyumbani Borussia Dortmund. Borussia haitakuwa na
wachezaji wake muhimu kama Marco Reus na Sven Bender ambao ni majeruhi,
pamoja na Mats Hummels ambaye alipata maumivu katika mchezo wa majaribio
wiki iliyopita.
Siku ya Jumatano itakuwa zamu ya Hamburg SV ikiikaribisha Bayern Munich ,
Bayer Leverkusen itakwaana na Kaiserslautern ya daraja la pili na
Hoffenheim inaikaribisha Wolfsburg.
Huko Uhispania Barcelona inaweza kukata tikiti yake katika fainali ya
kombe la mfalme , Kings Cup , Copa del Rey wiki hii kabla ya kuelekeza
mawazo yao katika Champions League.
Barca inakwaana na Real Sociedad siku ya Jumatano ambapo inaingia katika
mchezo huo ikiwa mbele kwa mabao 2-0 kutoka katika mchezo wa kwanza.
Real Madrid inakwenda ugenini kupimana ubavu na Atletico Madrid kesho
Jumaane, ambapo inaongoza pia kwa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza.
Huko mjini Sao Paulo nchini Brazil maafisa wamesema kuwa mashabiki
watatu wamejeruhiwa katika shambulizi la risasi baada ya mchezo
uliofanyika katika uwanja utakaofanyika michuano ya fainali za kombe la
dunia nchini Brazil mwishoni mwa juma. Mashabiki hao hata hivyo hawako
katika hali mbaya ya maisha yao.
No comments:
Post a Comment