Mazishi ya aliyekuwa msanii
maarufu wa filamu nchini Tanzania Steven Kanumba yamefanyika katika makaburi ya
Kinondoni mjini Dar es Salaam.
Steven Kanumba aliyefariki
dunia mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam amezikwa na maelfu ya
wakazi wa Jiji la Dar es Salaam,waliojikeza kuaga mwili kuuaga mwili wake
katika viwanja vya Leaders Club.
Makamu wa Rais wa Tanzania Dr
Ghalib Bilal aliwaongoza maelfu ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam
wanaokadiriwa kufikia elfu arobaini, kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa
msanii huyo kabla ya mwili wake kwenda kuzikwa.
Shughuli hiyo ya mazishi
ilisitishwa kwa muda baada ya umati huo wa watu kusongamana na kukosekana
udhibiti na utaratibu wa kuuga mwili huo.
Msanii Kanumba alijipatia
umaarufu mkubwa ndani na nje ya Tanzania kutokana na fani ya uigizaji wa filamu
za Kiswahili maarufu kama Bongo Movies.
Akizungumza kwa niaba ya
Serikali Waziri wa Habari,utamaduni,vijana na Michezo Dr Emmanuel John Nchimbi
amesema, ‘Tanzania imempoteza kijana shupavu aliyetumia vema kipaji chake
kujitafutia maendeleo na pia kuitangaza nchi yake.’
Kanumba alikuwa mbunifu
katika Fani ya Filamu. Juhudi zake zilimefikisha hadi Afrika Magharibi ambako
aliweza kuwashirikisha wasanii kadhaa maarufu kutoka Nigeria katika Filamu
zake.
Wakati huo huo Jeshi la
Polisi nchini Tanzania, linaendelea kumshikilia binti mmoja ambaye jeshi hilo
limemweleza kuwa alikuwa na Uhusiano wa Kimapenzi na Marehemu Steven Kanumba,
kwa maelezo kuwa alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu muda mfupi kabla ya
kifo chake.
Aidha uchunguzi wa Daktari
katika mwili wa marehemu bado unasubiriwa ili kujua chanzo cha kifo cha msanii
huyo. Polisi inasema uamuzi wa kumfungulia mashtaka Binti huyo utafuta baada ya
taarifa za daktari.
Kifo cha Msanii huyo Steven
Kanumba kimegusa hisia za wengi nchini Tanzania kiasi cha kuufanya msiba wake
kuwa na sura ya Kitaifa ambako hii leo barabara kadhaa jijini Dar es Salaam
zilifungwa kwa muda ili kupisha msafara wa mwili wa marehemu wakati ukielekea
kwenye viwanja vya Leader Club Kinondoni.
Mamia ya wananchi kutoka
pande mbali za jiji la Dar es Salaam walilazimika kutembea umbali mrefu kwa
miguu kwenda kutoa heshma zao za mwisho kwa msanii huyo aliyejizolea sifa
nyingi katika sanaa hiyo na wengi kuipenda na kuiheshimu kazi yake.
No comments:
Post a Comment