Mzunguko
wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara
unaanza kesho (Januari 26 mwaka huu) kwa raundi ya 14 ambapo timu 12
kati ya 14 za ligi hiyo zitakuwa katika viwanja sita tofauti.
Mabingwa
watetezi Simba watakuwa wenyeji wa African Lyon katika mechi
itakayochezwa saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Hiyo
itakuwa mechi ya kwanza kwa kikosi cha Simba tangu kiliporejea kutoka
Oman kwenye ziara ya mafunzo.
Pia
Kocha wake mpya, Mfaransa Patrick Liewig anatarajiwa kwa mara ya kwanza
kukiongoza kikosi hicho katika mechi ya VPL akisaidiwa na Moses Basena
na Jamhuri Kihwelo.
Mwamuzi
wa kimataifa Israel Mujuni ndiye atakayechezesha mechi hiyo ambapo
African Lyon inatarajiwa kuongozwa na Kocha Charles Otieno baada ya
kusitisha kibarua cha Pablo Velez kutoka Argentina kutokana na kufanya
vibaya katika mzunguko wa kwanza.
Uwanja
wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro wenye uwezo wa kumeza
watazamaji 8,000 ndiyo utakaohimili vishindo vya mechi kati ya Polisi
Morogoro na wenyeji Mtibwa Sugar. Polisi Morogoro ambayo ni ya mwisho
katika msimamo wa VPL ililazimisha suluhu katika mechi ya mzunguko wa
kwanza.
Coastal
Union ambayo kwenye dirisha dogo imesajili wachezaji sita akiwemo
Mzimbabwe Tinashe Machemedze itaoneshana kazi na wana-Tanga wenzao
Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.
Timu
zinazo katikati ya msimamo wa ligi, Ruvu Shooting na JKT Ruvu
zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani
ambapo sheria 17 zinazotawala mpira wa miguu zitakuwa chini ya usimamizi
wa refa Dominic Nyamisana kutoka Dodoma.
Wawakilishi
wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, Azam baada ya mechi
za kirafiki nchini Kenya wanarejea kwenye Ligi Kuu ya Vodacom kwa
kuikaribisha Kagera Sugar ya Kocha Abdallah Kibaden kwenye Uwanja wa
Chamazi.
Ni
mechi ya kulipa kisasi kwa Kagera Sugar baada ya kulala bao 1-0 katika
mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Septemba 15 mwaka jana Uwanja wa
Kaitaba, mjini Bukoba.
Maafande
wa Oljoro JKT wanaanza kuchanga upya karata zao katika mzunguko wa pili
kwa kuikaribisha Toto Africans ya Mwanza kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya
Sheikh Kaluta Amri Abeid, jijini Arusha.
Yanga
iliyopiga kambi ya mazoezi kwa takribani wiki mbili mjini Antalya,
Uturuki itaanza mzunguko wa pili dhidi ya Tanzania Prisons katika mechi
itakayochezwa keshokutwa (Januari 27 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Vinara
hao wa VPL wakiongoza kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya Azam
wanaowafuatia wanaikabili Tanzania Prisons ambayo imetumia dirisha dogo
kuongeza wachezaji wawili akiwemo mshambuliaji mkongwe Emmanuel Gabriel.
Timu
hizo zilitoka suluhu katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, jijini Mbeya. Hivyo kiu ya washabiki ni
kutaka kujua nani ataibuka mbabe kati ya timu hizo msimu huu.
Wakati
ameingiza wachezaji wawili kwenye dirisha dogo, Kocha wa Tanzania
Prisons, Jumanne Chale amempoteza David Mwantika katika dirisa hilo.
Beki huyo ametua katika timu ya Azam.
Msimamo kabla ya mapumziko ulikuwa hivi
Rnk | Team | MP | W | D | L | GF | GA | +/- | Pts | |
---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|
1 | Young Africans | 13 | 9 | 2 | 2 | 25 | 10 | 15 | 29 | |
2 | Azam | 13 | 7 | 3 | 3 | 17 | 11 | 6 | 24 | |
3 | Simba SC | 13 | 6 | 5 | 2 | 20 | 11 | 9 | 23 | |
4 | Mtibwa Sugar | 13 | 6 | 4 | 3 | 18 | 12 | 6 | 22 | |
5 | Coastal Union | 13 | 6 | 4 | 3 | 16 | 14 | 2 | 22 | |
6 | Kagera Sugar | 13 | 5 | 6 | 2 | 15 | 10 | 5 | 21 | |
7 | Ruvu Shooting | 13 | 6 | 2 | 5 | 19 | 17 | 2 | 20 | |
8 | Mgambo JKT | 13 | 5 | 2 | 6 | 10 | 13 | -3 | 17 | |
9 | JKT Ruvu | 13 | 4 | 3 | 6 | 13 | 20 | -7 | 15 | |
10 | JKT Oljoro | 13 | 3 | 5 | 5 | 13 | 16 | -3 | 14 | |
11 | Tanzania Prisons | 13 | 3 | 5 | 5 | 8 | 12 | -4 | 14 | |
12 | Toto African | 13 | 2 | 6 | 5 | 10 | 15 | -5 | 12 | |
13 | African Lyon | 13 | 2 | 3 | 8 | 9 | 20 | -11 | 9 | |
14 | Polisi Morogoro | 13 | 0 | 4 | 9 | 4 | 16 | -12 | 4 |
No comments:
Post a Comment