Ikiwa bado
watanzania na wadau mbalimbali wa mpira wa miguu wanaendelea kukumbuka raha ya
kupata matokeo mazuri uwanjani tena dhidi ya timu ngumu barani Afrika Cameroon na Zambia, bado kuna mambo mengi yakuzingatia kabla ya kufikia mafanikio zaidi huko mbele.
Hivi majuzi taifa Stars ambayo ambayo inadhaminiwa na kinywaji cha Kilimanjao, ilifanikiwa kuwaduwaza waliokuwa mabingwa wa soka barani Afrika Zambia maarufu 'Chipolopolo'
kwa kuwafunga bao 1-0 mchezo uliopigwa Disemba 22 mwaka jana, na juzi kwa mara nyingine tena watanzania
wakaendelea kufarijika tena na ushindi kama huo dhidi ya timu ngumu na yenye
wachezaji wakubwa na jina kubwa kisoka barani Afrika Cameroon, hiyo ikuwa ni michezo ya kimataifa ya kirafiki iliyochezwa katika siku ya kalenda ya shirikisho la soka duniani fifa(fifa date).
Huo si
ushindi mdogo hata kidogo ukizingatia ukubwa wa timu zenyewe na maumivu ya muda mrefu wanayopata
watanzania na ambayo yanaonekana kuwa sasa ni maumivu sugu kwani ni zaidi ya miaka 32 watanzania hawaja nusa wala kushiriki fainali za mataifa.
Ukiacha fainali hizo za Afrika, pia inaonekana ni kama ndoto ya alinacha kwa Tanzania kucheza fainali za kombe la dunia kiasi kuwa ni jambo la mazoea kuona tunatolewa katika harakati za michezo ya awali ya kufuzu fainali hizo na watanzania wa kizazi cha sasa kukata tamaa ya kuona yakitokea yale
yanayotokea Afrika kusini yanaijumuisha na Tanzania japo kwa kushiriki tu na si
kiushindani wa kupata taji la mataifa ya Afrika.
Hata hivyo
naamini kwa mapenzi ya mungu na kwa dua za watanzania wenye machozi yasiyofutika kila siku kutokana na kilio cha kutaka kuona taifa lao linashiriki fainali hizo iko siku maombi yao na dua zitajibiwa.
Naamini hivyo kwa kuwa waswahili wana msemo unaosema dalili ya mvua ni mawingu na endapo jitihada kidogo zikatumika kwa na malengo na dhamira chanya ya kweli hilo iko siku litatokea na pengine siku za hivi
karibuni.
Najaribu
kuugeuza msemo wa wahenga wa kale wa ‘mipango si matumizi’ na kuwa mipango ni
matumizi kwa maana ya tupange kutumia na kweli tutumie tulichonacho kwa mipango
sahihi na matumizi sahihi kwa nia sahihi halafu tuone mwisho wa siku nini
kitatokea.
Nampongeza
sana kocha Kim Poulsen ambaye kabla yake watanzania tulibugi kwa kumpa kazi
mrithi wa kocha wa kibrazil Marcio Maximo, Jan Poulsen ambaye kiukweli kama
tungeendelea na woga tuliokuwa nao wa kumuondoa basi hadithi ingebaki ileile
nafasi ya dhana ya msemo wa mipango si matumizi ingeendelea kututafuna.
Kocha Kim
Poulsen aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana alisoma vizuri njia
aliyopita Maximo na wapi alipokwama, ndipo alipopata majibu ya nini kilichomshinda
Jan Poulsen ambaye aliishusha Tanzania katika viwango vya ubora wa soka vinavyo
tambuliwa na shirikisho la soka duniani FIFA.
Anachokifanya
Kim ni kujaribu kujenga hali ya kujiamini kwa wachezaji vijana wanaocheza soka
nchini akichanganya na wachezaji wachache wazoefu kwa lengo kuongeza hali hiyo
ya kujiamini kwa vijana huku akitilia mkazo nidhamu ya kimchezo.
Anataka kuonyesha
uwezo wao lakini pia kubadilisha mtazamo wa utumwa wa mawazo kuwa Tanzania
hakuna mpira na kwamba ukicheza nje ya nchi hasa ulaya basi unakuwa bora.
Katika
hilo ameanza kueleweka sana na ama wachezaji wenyewe lakini pia na wadau mbalimbali wa
soka nchini.
Binafsi
sikuamini macho yangu nilipomuona Salum Abubakar ‘sureboy’, Amri Kiemba na
Frank Domayo na Mrisho Ngasa walivyokuwa wakicheza sehemu ya kiungo kwa
kujimini mbele ya kiungo mzoefu Pierre Wome aliyewahi kuchezea Roma, Bologna, Fulham,
Espanyol,Brescia Inter Milan na Verde Bremen pamoja Bedomo Henri wa Montpellier ya Ufaransa na
Nyom Allan wa Granada ya Hispania.
Sina maana
kwamba nimewadharau wachezaji hao wa Cameroon hapana, ninachotaka kusema hapo
ni ile hali ya kujimini kwa wachezaji wetu ukianza na mchezo dhidi ya timu ya
taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’ na juzi dhidi ya Cameroon, sasa hakuna matata kikosi kinajiamini sana na kinaweza.
Najua wako
wanaodhani kuwa pengine Cameroon walicheza soka ya kawaida na aina ya mchezo
wanaocheza siku zote, huo ni mtazamo wao, lakini pia wapo wanaodhani kuwa
kikosi chao kilikuwa hakijakamilika kwa kuwakosa nahodha Samweli Etoo na kiungo
wa Barcelona Alex Song hilo pia sitaki kubishana nalo inawezekana huo ni
mtazamo wa mtu, lakini mtazamo wangu ni kuwa ndani ya uwanja mpira ni ule ule tofauti
ni namna ya kuucheza na kufuata maelekezo ya kocha na kuzingatia nidhamu ya
mchezo kwa ujumla.
Kwa wachezaji wa timu ya taifa hilo wamelizingatia na hilo tumelishihudia katika mchezo wa juzi
dhidi ya Cameroon na hata mchezo wa mwezi Disemba dhidi ya Zambia, hivyo ndivyo
mpira wa miguu unavyochezwa duniani kote.
Falsafa ya
kocha Kim ni “Classy, Pride and character”.
Hapo anawataka wachezaji wa timu ya taifa kuonyesha madaraja yao ya uchezaji na
wanajivunia kuichezea timu ya taifa na pia kuonyesha kwamba wanaweza.
Pamoja na
hilo kocha Kim amekuwa akijivunia aina ya mchezo ambayo amekuwa akufundisha timu ya taifa kucheza mchezo wa pasi, kwenda mbele kutafuta nafasi na kufunga “Pass, move forward, open chances and score”.
Aina ya uchezaji tumeishuhudia katika michezo hiyo miwili iliyopita ambapo
wachezaji wamekuwa wakishirikiana katika maeneo yote matatu kwa maana ya ulinzi
ambapo ngome ya taifa sasa imekuwa ngumu mithili ya ukuta wa Berlin ni ngumu kupenyeka
kirahisi.
Pia tumeishuhudia timu ya taifa ambayo inacheza mpira wa kufungua na
kupeana pasi , kwenda mbele kufungua nafasi na kufunga magoli ukiachilia mbali
makosa madogo madogo ya kiuchezaji ambayo yamekuwa yakionekana ambayo ama
yanasababishwa na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja au umakini mdogo na si nidhamu
ya mchezo.
Pia wamekuwa wakicheza kitimu zaidi ambapo wakipoteza mpira wote wanashirikiana kuutafuta mpira uliopotea na wanapounasa wanaanza kwa kujipanga kwa mtindo ule ule wa kupiga pasi, kufungua nafasi na kushambulia kwa lengo la kufunga goli, hivyo ndivyo mpira wa miguu wa kisasa unavyochezwa, nukuu ya kocha Kima anasema hiyo ni 'character ya uchezaji na mchezaji'.
Lakini pia tukumbuke uwanjani kuna wachezaji wa upande wa pili 11
ambao nao wana mbinu zao za kuzuia na kushambulia.
Niwa wazi
sasa mambo yameanza kuwa mazuri, lakini wasiwasi wangu ni je wachezaji wenyewe
nje ya uwanja wanajitunza? Wanajua kuwa wanadhamana na kubadilisha historia ya
nchi katika mchezo wa soka? Na jamii inashiriki vipi kuwalinda kwa maslahi ya
nchi.
Upande wa
pili ni katika vilabu wanavyotoka wachezaji wetu wanajua kuwa nidhamu yao ya
kiuchezaji katika timu ya taifa inaanzia huko? Na nini wafanye kulinda nidhamu
yao na viwango vyao. Kocha Kim anasema UMOJA NI NGUVU.
Tushirikiane sote wachezaji,
makocha,TFF, wadau, Serikali na jamii kwa ujumla kuhakikisha mipango yetu
inakuwa matumizi na dhamira yetu ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika na
kombe la dunia inafanikiwa tukianza na mchezo wetu wa mwezi ujao dhidi ya timu ya Taifa ya Morroco.
Huo ni mchezo muhimu wa hatua ya makundi kusaka kufuzu kombe la dunia tukiwa katika kundi C na kwasasa taifa stars ikiwa katika nafasi ya pili ya kundi hilo ikiwa na alama 3 baada ya kucheza michezo miwili.
Kundi hili timu nne za Ivory Coast, Morroco na Gambia linaongozwa na Ivory Coast yenye alama 4.
Stars ilianza kwa kuwafunga Gambia bao 2-1 uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam kabla kufungwa na Ivory Coast bao 2-0 jijini Abidjan michezo iliyochezwa mwezi june mwaka jana, sasa unasubiriwa mchezo wa tarehe 22 mwezi ujao dhidi ya Morroco.
Huo ni mchezo muhimu kwa timu ya taifa ya nchi yetu, hivyo ni muhimu tukafanya maandalizi makubwa kwa kuwa tunacheza nyumbani, basi matokeo yawe ya ushindi mnono kwani kikosi cha Stars sasa bado kina moto na hakuna wa kumuogopa tena.
Tuwatazame wenzetu
kama Cape Verde, Bukina Faso na Ethiopia na wengine ambao walikuwa nyuma katika
soka lakini sasa wanatengeneza historia mpya katika mataifa yao, Afrika na
dunia kwa ujumla katika maendeleo ya soka.
Ombi langu kwa wachezaji wenyewe ambao ndio
tegemeo la watanzania ni kuongeza hali ya kujiamini na kujitunza kimazoezi kila
siku na kila wakati kama kweli wana malengo binafsi ya kwenda mbali zaidi
lakini pia kama wanataka kuandika historia ndani ya nchi yao basi huu ni
wakati wa kufanya hivyo.
No comments:
Post a Comment