10 WAKATA RUFANI KAMATI YA RUFANI YA UCHAGUZI TFF
RUFANI
kumi zimewasilishwa mbele ya Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi
ya TFF kuhusiana na uchaguzi utakaofanyika Februari 22 na 24 mwaka huu.
Wakati
uchaguzi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) utafanyika Februari
22 mwaka huu, ule wa TFF wenyewe utafanyika Februari 24 mwaka huu.
Waliowasilisha
rufani mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Idd Mtiginjola ni pamoja na
waombaji uongozi saba walioenguliwa katika kinyang’anyiro hicho.
Warufani hao ni Omari Mussa Nkwarulo na Michael Richard Wambura
walioomba kugombea urais na umakamu wa rais.
Wengine
ambao waliomba ujumbe wa Kamati ya Utendaji kuwakilisha kanda
mbalimbali ni Farid Nahdi (Morogoro na Pwani), Mbasha Matutu (Shinyanga
na Simiyu), Omari Isack Abdulkadir (Dar es Salaam), Eliud Peter Mvella
(Iringa na Mbeya) na Shaffih Kajuna Dauda (Dar es Salaam).
Warufani
wengine ni wadau ambao waliweka pingamizi dhidi ya baadhi ya waombaji
uongozi katika TPL Board na TFF, pingamizi ambazo zilitupwa mbele ya
Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa sababu za kiufundi.
Wadau
hao waliokata rufani ni Agape Fue dhidi ya Kamati ya Uchaguzi TFF
kupinga kumpitisha Jamal Malinzi kugombea urais, Medard Justinian dhidi
ya Kamati ya Uchaguzi TFF kupinga kumpitisha Athuman Nyamlani kugombea
urais, na Frank Mchaki dhidi ya Kamati ya Uchaguzi TFF kupinga
kumpitisha Hamad Yahya kugombea uenyekiti wa TPL Board.
Kamati
ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF imetoa siku ya kesho (Februari 9 mwaka
huu) kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 8 mchana kwa wote wenye maslahi na
rufani hizo (interested parties) kupitia rufani hizo na kuwasilisha hoja
zao kwa maandishi.
Kwa
watakaoshindwa kufanya hivyo watapata fursa ya kuwasilisha hoja zao kwa
mdomo, ambapo wanaweza kuwa wenyewe au wanasheria wao siku ya
usikilizwaji wa rufani hizo. Rufani zitasikilizwa Jumapili (Februari 10
mwaka huu) kuanzia saa 2 asubuhi.
No comments:
Post a Comment