Meneja wa Manchester United, David Moyes amedai kuwa
timu yake inacheza dhidi ya waamuzi pamoja na timu pinzani baada ya
kushuhudia vijana wake wakipoteza mchezo dhidi ya Sunderland katika
mechi ya nusu fainali ya kombe la Capital One.
Kocha huyo wa Manchester United alisikitishwa na
uamuzi wa kuipatia Sunderland penalti na hivyo kuiwezesha kuibuka na
ushindi wa mabao 2-1.
"Tunacheza dhidi yao(waamuzi) na timu pinzani kwa wakati mmoja," ameiambia Sky Sports.
"Kwa kweli inatisha. Tunaanza kuwacheka kutokana na maamuzi wanayotoa."
Mwaamuzi wa mchezo kati ya Manchester United na
Sunderland, Andre Marriner aliwapa penalti wenyeji akishauriwa na mmoja
wa wasaidizi wake baada ya Adam Johnson kuanguka katika eneo la hatari
alipokabiliana na Tom Cleverley wa Manchester United.
Sunderland iliongoza kipindi cha kwanza cha
mchezo kupitia kwa Ryan Giggs, aliyejifunga goli. Japokuwa Nemanja Vidic
aliisawazishia timu yake mara baada ya kuanza kipindi cha pili, penalti
iliyotolewa kwa vijana wa Borini, kunawapa Paka Weusi hao, "Black Cats"
kuingia na ushindi katika mchezo wa marudiano utakaopigwa tarehe 22
Januari katika uwanja wa Old Trafford.
Katika kipindi cha wiki moja, Manchester United
imeshuhudia kipigo kingine katika michezo ya kuwania vikombe huko
England. Timu hiyo tayari imeng'olewa katika mashindano ya kuwania kombe
la FA baada ya kucharazwa mabao 2-1 na Swansea.
Mapema mwezi huu Moyes alisema ilikuwa "kashfa"
kwa Manchester United kunyimwa penalti dakika za mwisho katika mechi yao
ya kuwania ubingwa wa ligi kuu ya England dhidi ya Tottenham. Katika
mchezo huo uliofanyika uwanja wa Old Trafford, Manchester United
ilitunguliwa mabao 2-0.
Hii ni mara ya kwanza kwa Manchester United tangu tarehe 22-26 Aprili 1992 kupoteza michezo mitatu ndani ya wiki moja.
No comments:
Post a Comment