Timu ya taifa ya vijana umri chini
ya miaka kumi na saba (U.17) Serengeti Boys, imeelekea mkoani Mbeya kuendelea na maandalizi ya kufuzu fainali za vijana
zitazofanyika nchini Morocco mwaka 2013. Timu hiyo imepangiwa kupambana
na timu ya taifa ya vijana wa Misri (Egypt) katika hatua inayofuata,
pambano ambalo linatarajia kufanyika Oktoba 2012. Timu hiyo ilipata
ushindi baada ya timu ya vijana ya Kenya kujitoa kwenye michuano hii.
Timu hiyo
imekwenda Mbeya kwa mwaliko wa Chama cha Mpira wa Miguu cha
Wilaya ya Mbeya Mjini (MUFA) na ikiwa huko chama hicho kitaihudumia kwa
malazi, chakula na huduma nyingine ndogondogo. Timu inategemea kupangiwa
michezo kadhaa ya majaribio na timu kabambe za mkoani humo ikiwemo
Mbeya City, Tanzania Prisons na timu za kombaini.
Shirikisho
la Mpira wa Miguu nchini linapenda kutumia fursa
hii kuishukuru na kuipongeza MUFA, kwa kuonyesha mfano unaostahili
kuigwa na wadau wengine, wa kushirikiana katika maandalizi ya kuziandaa
timu zetu za taifa. Kitendo hicho kinaonyesha kuguswa, uwajibikaji,
uzalendo na ukomavu katika kutatua matatizo kwa vitendo na sio kwa
lawama bila suluhisho.
Shirikisho
pia linaishukuru benki ya NMB kwa kutoa msaada wa jezi seti moja na
fedha sh. Millioni tano, zilizowezesha vijana hawa kupata posho zao za
kambi na kusafiri kwenda Mbeya. Itakumbukwa kuwa benki ya NMB imekuwa na
mchango mkubwa sana katika maendeleo ya soka ya vijana kwa muda mrefu
sasa. Kwa kipindi cha miaka sita (2006-2010) iliyopita ilidhamini
mafunzo ya makocha wanaojihusisha na program za maendeleo ya vijana
nchini, vilevile ilitoa mipira ya program za vijana kwa vyama vya mikoa.
Hivyo tunaishukuru kwa kuthamini mchango wao huo na kwa kuendelea kutoa
msaada ili kuhahakisha inalinda mafanikio ya program hizo.
Shirikisho
linapenda kuwaomba wadau wengine kujitokeza kusaidia kuwaandaa vijana
wetu hawa pekee waliobaki kwenye mashindano. Mafanikio ya timu yetu ya
taifa (Taifa Stars) siku za usoni yanategemea sana msingi bora wa vijana
hawa. Hivyo ni vema tukashirikiana kama walivyojitokeza MUFA na NMB.
Hutisiti
kueleza bayana kuwa kama si wadau hawa kambi ya vijana ilikuwa
inavunjika, na baada ya kurudi Mbeya kama hakutakuwa na wadau wengine
watakaojitokeza basi uwezo wa kuendelea na kambi ya maandalizi kwa
vijana wetu utakuwa finyu mno.
Shirikisho
lina imani kuwa wakazi wa Mbeya watatoa ushirikiano wa hali ya juu
wakiongozwa na Chama cha Mpira cha Mkoa (MREFA), kwa Serengeti Boys ili
kufanikisha maandalizi hayo.
No comments:
Post a Comment