KWA MAWASILIANO ZAIDI TUMIA BARUA PEPE rockersports212@yahoo.com AU TUPIGIE KUPITIA NAMBARI 0767166607 AU 0717166607. KARIBU SANA. 66666666607 AU 0717166607

Thursday, April 17, 2014

Azam waanza kujinoa kukamilisha ligi dhidi ya JKT Ruvu

AZAM FC imeanza mazoezi jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam baada ya mapumziko ya siku moja, tangu wachezaji wa timu hiyo warejee kutoka Mbeya ambako walitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwishoni mwa wiki.

Azam inatarajiwa kucheza mechi ya mwisho ya kukamilisha msimu wa ligi Jumamosi Uwanja wa Azam Complex dhidi ya JKT Ruvu, siku ambayo pia watakabidhiwa taji lao la ubingwa wa Ligi Kuu.

Azam ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Jumapili, baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-1 Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, huku waliokuwa wapinzani wao katika mbio za taji hilo, Yanga SC wakishinda 2-1 dhidi ya JKT Oljoro mjini Arusha.

Azam imefikisha pointi 59 ikiwa na mchezo mmoja mkononi ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote baada ya mechi za mwisho Aprili 19, mwaka huu. Yanga SC yenye pointi 55 sasa ikiifunga Simba SC wiki ijayo itafikisha 58.

Licha ya kuwa timu ya kwanza kuifunga Mbeya City kwenye Uwanja wake Aprili 13, mwaka huu, Azam FC pia inakuwa timu ya kwanza nje ya Simba na Yanga kutwaa ubingwa wa Bara tangu mwaka 2000 Mtibwa Sugar ilipofanya hivyo.

Azam inakuwa timu ya saba nje ya Simba SC kutwaa taji la Ligi Kuu, baada ya Cosmo mwaka 1967, Mseto mwaka 1975, Pan Africans mwaka 1982, Tukuyu Stars mwaka 1986, Coastal Union 1988 na Mtibwa Sugar mara mbili mfululizo 1999 na 2000.

No comments:

Post a Comment