Rais Dilma Rousseff amewaomba Wabrazil kuungana pamoja kwa ajili ya
Kombe la Dunia la 2014, akisema taifa liko tayari. Migomo na maandamano
kuhusiana na gharama za maandalizi vinatishia tamasha hilo
Rais Rousseff amewataka Wabrazil kuwa na matumaini kuhusiana na dimba la
mwaka huu la Kombe la Dunia, akisema mafanikio ya kuandaa
kinyang'anyiro hicho yatauwakilisha ushindi wa ari ya taifa.
Katika hotuba yake iliyorushwa kwenye televisheni kabla ya ufunguzi wa
tamasha hilo, rais huyo amesema macho ya ulimwengu mzima yanaiangazia
Brazil akisema nchi hiyo ilikabiliana na vizingiti vikuu na sasa iko
tayari ndani na nje ya viwanja.
Rousseff ameihutubia moja kwa moja timu ya taifa "selecao"
akiwaambia wachezaji kwamba “katika hayo mavazi ya rangi za kijani na
njano, mnadhihirisha historia ya watu wa Brazil”.
Kitisho cha migomo na maandamano
Wakati huo huo, kitisho kilichokuwepo cha mgomo kimeondolewa kwa muda
huku wafanyakazi wa treni za chini ya ardhi mjini Rio wamekifutilia
mbali mgomo wao baada ya kupewa nyongeza ya mshahara ya asilimia 8.
Mgomo wa siku tano wa usafiri mjini Sao Paolo pia ulisitishwa Jumatatu
wiki hii, ijapokuwa huenda ukarejea tena wakati michuano itakapoanza
kama wafanyakazi waliopigwa kalamu hawatorudishwa kazini.
Sherehe za ufunguzi wa dimba hilo zinaandaliwa katika uwanja wa
Corinthians Arena, mjini Sao Paulo, na miongoni mwa wageni
watakaohudhuria ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon pamoja na
viongozi 12 wa nchi na serikali.
Lakini kabla ya kuziona timu zao zikimenyana viwanjani,
mashabiki wanaowasili nchini Brazil kwanza watalazimika kupambana na
mparaganyiko katika viwanja vya ndege, pamoja na foleni za taxi za hadi
saa mbili.
Viwanja vya ndege vinajiandaa kuwakaribisha mamilioni ya
wasafiri wa kimataifa wanaotua nchini humo kwa ajili ya tamasha hilo
kubwa la soka. Maafisa wa Brazil wanasisitiza kuwa watakuwa tayari,
lakini abiria huenda wakajikuta katika hali ngumu.
Timu zote 32
zimewasili nchini humo tayari kushuka dimbani kupambana na wapinzani.
Brazil dhidi ya Croatia
Baada ya sherehe za ufunguzi, vijana wa kocha Luiz Felipe Scolari,
maarufu kama “SELECAO” watashuka dimbani kupambana na Croatia katika
mechi ya ufunguzi ya Kundi A. Na kama wenyeji hao wataweza kufika katika
fainali na kunyakua taji hilo mnamo Julai 13, watakuwa timu ya tatu
pekee iliyocheza mechi ya ufunguzi kuwahi kufanya hivyo.
Katika vinyang'anyiro 19 vya Kombe la Dunia, ni Italia pekee mnamo mwaka
wa 1934 na England mwaka wa 1966 zilizowahi kucheza mechi ya kwanza na
baadaye kushinda katika fainali.
No comments:
Post a Comment