Azam FC vs Mtibwa Sugar; Ripoti kamili ya mchezo, Jabir Aziz, Himid Mao wafunika kwa pressing za kufa mtu
Goli pekee la mshambuliaji wa kimataifa wa Azam FC, Tchetche Kipre limeipatia timu hiyo ushindi dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa ligi kuu uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.
Azam FC imepata pointi tatu na kufikisha jumla ya pointi 7 katika msimamo wa ligi kuu baada ya kupata ushindi wa 1-0, katika michezo yake ya mwanzo, ilishinda michezo mmoja na kutoka sare mchezo mmoja.
Mchezo huo uliokuwa na sura ya ushindani Azam FC ilitaka kulipa kisasi cha kufungwa 2-1 na Mtibwa katika mchezo ulirudiwa msimu uliopita, timu zote zilicheza kandanda safi katika vipindi vyote viwili.
Ushindi huo wa Azam FC ulianza kutafutwa mapema katika sekunde ya 45 ya mchezo huo ambapo walifanya shambulizi lakini mshambuliaji John Bocco alipiga mpira ukatoka nje.
Mashambulizi yaliendelea kuliandama lango la Mtibwa, dakika ya nane Ibrahim Mwaipopo alipiga mpira wa adhabu ukatoka nje mita chache karibu na goli la Mtibwa, dakika ya 15 Abdi Kassim ‘Babi’ alijaribu kwa kupiga mpira wa adhabu ukaokolewa na kipa Shaaban Kado wa Mtibwa.
Dakika ya 29 Kipre aliipatia goli la kwanza na pekee katika mchezo huo akimalizia kazi nzuri ya Ibrahim Mwaipopo na kutumia uzembe wa beki ya Mtibwa na kupiga mpira kiufundi uliotinga moja kwa moja wavuni.
Goli hilo lilizipeleka timu zote mapumziko Azam FC ikiongoza 1-0 dhidi ya Mtibwa, kipindi cha pili timu zote zilianza mchezo kwa kasi ambapo Mtibwa Sugar walijaribu kufanya mashambulizi ya kurudisha goli hilo lakini walizini wa Azam FC walizuia mashambulizi hayo.
Timu zote zilifanya mabadiliko Azam FC alitoka Abdi Kassim nafasi yake ikachukuliwa na Michael Bolou dk 62, dakika ya 84 Jabir Aziz alirejea benchi na nafasi yake kuchukuliwa na Khamis Mcha na Gaudence Mwaikimba aliingia kumpumzisha Himid Mao katika dakika ya 90, mabadiliko hayo yaliimarisha kikosi hicho lakini hayakuongeza goli lingine.
Wachezaji Jabir Aziz na Himid Mao walicheza kwa kujituma na kwa nguvu muda wote waliokuwepo uwanjani wakifanya kile kinachoitwa kitaalam "Pressing" haikushangaza kuona wakifanyiwa mabadiliko. Jabir baada ya kuumizwa mara kadhaa na Himid Mao kutokana na kuchoka.
Mtibwa watajutia nafasi walizopata wachezaji Jamal Mnyate dk 37 alipiga mpira ukaambaa goli la Azam FC na kutoka nje na dk 41 alipiga shuti likaokolewa na kipa Mwadini Ally wa Azam FC, Shaban Kisiga katika dk 83 akiwa yeye na lango la Azam FC alishindwa kuipatia timu yake goli baada ya kupiga mpira uliodakwa na kipa Mwadini.
Katika mchezo huo beki wa Mtibwa, Salvatory Ntebe alitolewa kwa kadi nyekundu katika dakika ya 62 na mwamuzi Ibrahim Kidiwa wa Tanga, baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano kwa kumwangusha Kipre Tchetche dakika ya 50 na dk 61 kumpiga kiwiko.
Azam FC inajiandaa na mchezo wake wanne utakaochezwa wiki ijayo dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa na kuonyeshwa moja kwa moja na kituo cha Super Sport.
Kikosi Azam FC Mwadini Ally, Aggrey Moris, Erasto Nyoni, Samir Haji Nuhu, Said Morad, Himid Mao/Gwaudence Mwaikimba 90’, Ibrahim Mwaipopo, Abdi Kassim ‘Babi’/Michael Bolou 62’, Jabir Aziz/Khamis Mcha 84’, John Bocco na Tchetche Kipre.
Mtibwa Shaba Kado, Malika Ndeule, Dickson Daud, Issa Radhid ‘Baba Ubaya’, Awadh Juma, Shaban Nditi, Salvatory Ntebe (red card 61), Shaban Kisiga, Jamal Mnyate/Ally Mohamed, Vincent Barnabas/Babu Ally na Hussein Javu/Mohamed Mkopi.
No comments:
Post a Comment