1. Kamati
ya Uchaguzi ya TFF katika kikao chake kilichofanyika tarehe 03-04
Oktoba 2012 ilijadili michakato ya chaguzi za vyama vya mpira wa miguu
vya Mikoa ya Rukwa (RUREFA), Arusha (ARFA), Shinyanga (SHIREFA), Pwani
(COREFA), Dar es Salaam (DRFA) na Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu
Tanzania (FRAT). Kamati iliamua yafuatayo:
(a) Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Arusha (ARFA)
Uchaguzi wa ARFA utafanyika Jumapili, tarehe 07 Oktoba 2012 mjini Arusha kama ulivyopangwa.
(b) Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT)
Uchaguzi wa FRAT utafanyika Jumapili, tarehe 07 Oktoba 2012 mjini Dodoma kama ulivyopangwa.
(c) Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA)
Uchaguzi wa COREFA utafanyika Jumapili, tarehe 14 Oktoba 2012 Wilayani Mafia kama ulivyopangwa.
(d) Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA)
Kamati
ilibaini na kujiridhisha kuwa kulikuwa na udanganyifu uliofanywa na
Kamati ya Utendaji ya RUREFA katika kutekeleza majukumu yake ya kikatiba
hususan, uteuzi wa baadhi ya wajumbe wa Kamati
ya Uchaguzi ya RUREFA. Pamoja udanganyifu huo, Kamati ya Uchaguzi ya TFF
imejiridhisha kuwa Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA imeshindwa kutimiza
wajibu wake katika kusimamia uchaguzi wa RUREFA, hata baada ya kuwa
imepewa onyo kuzingatia matakwa ya Kanuni za Uchaguzi.
Kutokana
na udanganyifu uliofanyika katika uteuzi wa baadhi ya wajumbe wa Kamati
ya Uchaguzi ya RUREFA, Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 26(2) na (3) na Katiba ya TFF Ibara ya 49(1), imeamua yafuatayo:
(i) Imeifuta
Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA. TFF itateua Kamati mpya ya Uchaguzi ya
RUREFA itakayoandaa na kusimamia uchaguzi wa RUREFA.
(ii)Uteuzi
wa Kamati mpya ya Uchaguzi ya RUREFA utafanyika wakati muafaka baada ya
TFF kukamilisha taratibu za uteuzi, na ratiba ya uchaguzi ya RUREFA
itatangazwa baada ya zoezi hilo.
(e) Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA)
Kamati
ya Uchaguzi ya TFF imebaini kuwa baadhi ya viongozi wa Kamati ya
Utendaji ya SHIREFA wanaingilia mchakato wa uchaguzi wa SHIREFA kinyume
na matakwa ya Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa
TFF. TFF haitambui maamuzi ya uongozi wa SHIREFA wa kuivunja Kamati ya
Uchaguzi ya SHIREFA inayosimamia uchaguzi wa Chama hicho. Zoezi la
uchaguzi wa SHIREFA lililoanza tarehe 08 Septemba 2012 linaendelea na
uchaguzi wa viongozi wa SHIREFA utafanyika tarehe 20 Oktoba 2012 kama
ulivyopangwa.
(f) Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es salaam (DRFA)
Kamati
ya Uchaguzi ya TFF itakamilisha zoezi la kusikiliza rufaa zilizokatwa
dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na kupitia mchakato mzima wa
uchaguzi wa DRFA, ili kujiridhisha kama matakwa ya Katiba ya DRFA na
TFF yamezingatiwa. Kamati ya Uchaguzi itatoa uamuzi kuhusu rufaa
zilizowasilishwa kwenye Kamati kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za
wanachama wa TFF na kuhusu mchakato wa uchaguzi wa DRFA baada ya kikao
chake kitakachofanyika Jumanne, tarehe 09 Oktoba 2012.
2. Kuzingatia Kanuni za Uchaguzi:
(i) Kamati
ya Uchaguzi ya TFF itaishauri Mamlaka husika ya TFF kuwachukulia hatua
za kinidhamu viongozi wa Kamati za Utendaji walioko madarakani
wanaoingilia michakato ya chaguzi za wanachama wa TFF na kusababisha
mikanganyiko katika chaguzi ili ama wandelee kuwa madarakani kinyume na
matakwa ya Katiba ya TFF Ibara ya 12(2)(a) au wapitishwe kugombea
uongozi kinyume na taratibu zilizowekwa na TFF.
(ii)Kamati
ya Uchaguzi ya TFF inasisitiza na kuzitaka Kamati za Uchaguzi za vyama
wanachama wa TFF kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF
wakati wote wa michakato ya uchaguzi wa viongozi wa vyama hivyo.
Angetile Osiah
KATIBU MKUU
KATIBU- KAMATI YA UCHAGUZI –TFF
SERENGETI BOYS KUVUNJA KAMBI KWA MECHI
Timu
ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) ambayo
imepata tiketi ya kucheza raundi ya tatu ya michuano ya Afrika baada ya
Misri kujitoa itavunja kambi yake kwa mechi ya kirafiki dhidi ya kikosi
cha Yanga cha U20.
Mechi
hiyo itachezwa kesho (Oktoba 6 mwaka huu) Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni. Kiingilio kwenye mechi
hiyo kitakuwa sh. 2,000 tu.
TAFCA YAONGEZA MUDA WA KUCHUKUA FOMU
Kamati
ya Uchaguzi ya Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA)
imeongeza muda kwa wagombea kuchukua fomu kwa ajili ya uchaguzi wa chama
hicho utakaofanyika katikati ya mwezi ujao.
Kwa
mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA, Ramadhan
Mambosasa, jana ndiyo ilikuwa mwisho wa kuchukua fomu lakini mwitikio wa
wagombea umekuwa mdogo ambapo ni watano tu waliojitokeza.
Hivyo,
amesema wameongeza muda wa kuchukua na kurudisha fomu ambapo mwisho
itakuwa ni Oktoba 9 mwaka huu saa 10 kamili alasiri. Fomu zinapatikana
ofisi za TAFCA ambazo ziko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es
Salaam.
Nafasi
zinazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu
Msaidizi, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, Mhazini na wajumbe watatu wa
Kamati ya Utendaji.
No comments:
Post a Comment