Msemaji wa TFF Bonface Wambura |
CHAMA cha Waandishi wa
Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinampongeza mwanachama wake Boniface
Wambura kwa kuteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) kuwa
mmoja wa maofisa watakaoshughulikia masuala ya habari wakati wa fainali za
Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zitakazofanyika nchini Equatorial Guinea.
TASWA imepokea kwa furaha
uteuzi huo wa Wambura ambaye ni Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) na inaamini ataendelea kufanya vizuri kama anavyotekeleza majukumu yake
ya kazi ndani ya TFF.
Tangu Wambura aanze kazi ya
Ofisa Habari wa TFF kumekuwa na mapinduzi makubwa yanayohusiana na mambo ya
habari na katika hili waandishi wa habari za michezo nchini ni mashahidi wa
hilo kwani amekuwa mtu sahihi kwao na amekuwa na ushirikiano mkubwa usio na
kifani kwa wanahabari wenzake.
Kwa vile Wambura ni
mwanachama wetu hai wa TASWA, kwa kuteuliwa kwake huko ni faraja kwa chama na
tunamtakia kila la heri ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake kwani hiyo ni
ishara tosha kwamba kazi yake inaonekana na inathamanika.
Wambura ameteuliwa na Rais
wa CAF, Issa Hayatou kwa ajili ya kufanikisha uendeshaji wa fainali hizo za
Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zilizopangwa kuanza Oktoba 28, 2012 na kumalizika
Novemba 11, 2012, ambapo atakuwa mmoja wa maofisa watatu watakaoshughulikia
habari kwenye fainali hizo. Wengine ni ofisa kutoka makao makuu ya CAF, Mahmoud
Garga na Arlindo Macedo kutoka Angola.
WAKATI HUOHUO
B: Mkutano Mkuu wa TASWA
Sekretarieti ya TASWA
imefikia hatua ya mwisho ya mazungumzo na mdhamini wa Mkutano Mkuu unaotarajiwa
kufanyika mwezi ujao katika tarehe ambayo itatangazwa rasmi.
Kamati ya Utendaji ya TASWA
ilikubaliana katika kikao chake mwezi uliopita kuwa Mkutano Mkuu wa TASWA mwaka
huu uwe wa aina yake kwa kuwawezesha wanachama kukaa pamoja na kubadilishana
mawazo na ikashauri ikiwezekana ufanyike nje ya Dar es Salaam kama hali
itaruhusu.
Kutokana na hali hiyo,
kikao kiliiagiza sekretarieti ya TASWA itafute mdhamini wa kufanikisha suala
hilo na kwamba kama ikishindikana mkoani ifanyike Dar es Salaam lakini kuwe na
mdhamini.
Tayari hilo limefanyika na
mdhamini amepatikana, ambapo hatua ya mwisho ya mazungumzo na mdhamini itakuwa mapema
wiki ijayo na baada ya hapo itatangazwa
tarehe rasmi.
Nichukue nafasi hii
kuwaomba wanachama ambao hawajalipa ada zao wafanye hivyo kwa kuwasiliana na
Mhazini wa chama au Mhazini Msaidizi ili waepuke usumbufu wa kushindwa kuhudhuria
mkutano huo.
Nawasilisha
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
25/10/2012.
No comments:
Post a Comment