Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba jioni ya leo watakuwa na kibarua pevu cha kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa sugar ya Turiani Morogoro mchezo utakao pigwa uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.
Huu ni mchezo wa mwisho wa Simba katika ligi kuu ya soka Tanzania Bara kabla ya kuelekea nchini Angola kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya FC Libolo.
Simba itakuwa inaingia uwanjani hii leo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa ba0 1-0 iliyoupata jijini Mbeya mbele ya Tanzania Prison ushindi ambao ulifakiwa kutuliza hali ya hewa kufuatia matokeo ya sare mbili mfululizo toka JKT Oljoro na JKT Ruvu tangu kuanza kwa ligi mzunguko wa pili wa ligi hiyo.
Kocha mkuu wa wekundu hao mfaransa Patrick Liewig ambaye yuko katika shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo la kutakiwa kung'olewa kutokana na mashabiki kuanza kuhoji juu ya uwezo wake, atalazimika kuendelea kumtumia Juma Nyoso katika sehemu ya ulinzi wa kati akicheza pacha na Komabil Keita kufuatia mlinzi mahiri Shomari Kapombe kutokuwa katika hali nzuri kimchezo baada ya kufanyiwa matibabu ya kuondoa damu iliyovilia ndani ya mishipa.
Taarifa iliyotolewa jana na msemaji wa klabu hiyo Ezekiel Kamwaga imesema kuwa Kapombe hatakuwemo katika kikosi cha leo na kwamba huenda akarejea uwanjani katika mchezo wa marudiano dhidi ya Libolo nchini Angola.
Simba endapo itashinda katika mchezo leo itakuwa imefanikiwa kufikisha jumla ya alama 34 na hivyo kuwa nyuma kwa tofauti ya alama 2 dhidi ya Azam fc yenye alama 36 baada ya jana kutota mbele ya mabingwa soka Afrika mashariki na kati Yanga kwa kufungwa bao 1-0 na hivyo kuifanya Yanga kuendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na alama 39.
Kwa upande wao Mtibwa Sugar ambao katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa ligi hiyo kule mkoani Morogoro katika dimba la Jamhuri walifanikiwa kuwaonjesha joto ya jiwe Simba kwa kuwafunga mabao 2-0, na kuanza kuchafua hali ya hewa ya Msimbazi, hii leo watakuwa wakitaka kudhihirisha umwamba wao mbele ya Simba kwa kuwafunga mara mbili, jambo ambalo litaufanya mchezo huo kuwa mgumu.
No comments:
Post a Comment