Mkutano Mkuu
Maalumu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) uliofanyika leo (Julai 13 mwaka
huu) umepitisha marekebisho ya Katiba yake, hivyo mchakato wa uchaguzi
unatarajia kuanza wakati wowote.
Wajumbe
zaidi ya 100 walihudhuria Mkutano huo uliofanyika ukumbi wa NSSF Waterfron, Dar
es Salaam na kufunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera aliyewataka
wajumbe kuhakikisha kiwango cha mpira wa miguu nchini kinakuwa.
Mkutano huo
uliokuwa chini ya uenyekiti wa Rais wa TFF, Leodegar Tenga umefanya marekebisho
ya Katiba kutokana na maelekezo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA). James Johnson kutoka Idara ya Wanachama ndiye aliyeiwakilisha FIFA
katika mkutano huo.
Aprili mwaka
huu FIFA ilisimamisha mchakato wa uchaguzi wa TFF, na kuagiza kwanza yafanyike
marekebisho ya Katiba ili kuingiza Kamati ya Maadili, na Kamati ya Rufani ya
Maadili ambavyo ndivyo watashughulikia matatizo ya kimaadili kwa familia ya
mpira wa miguu nchini.
Mbali ya
kamati hizo, mabadiliko hayo pia yametengeneza ngazi mbili za kushughulikia
masuala ya kinidhamu ambazo ni; Kamati ya Nidhamu na Kamati ya Rufani ya
Nidhamu.
Kamati ya
Utendaji ya TFF chini ya Rais Tenga itakutana kesho (Julai 14 mwaka huu) kwa
ajili ya kuteua wajumbe watakaounda Kamati hizo ili kuruhusu kuanza mchakato wa
uchaguzi ambao FIFA iliusimamisha hadi vitakapoundwa vyombo hivyo.
No comments:
Post a Comment