Mpira uliopigwa kwa kichwa na Stefan Kiessling Leverkusen uliingia langoni kupitia nje ya wavu. |
Mahakama ya michezo ya Shirikisho la Soka Ujerumani DFB imetoa uamuzi
kuwa mechi kati ya Hoffenheim na Bayer Leverkusen iliyozingirwa na bao
lenye utata haitarudiwa
Mahakama hiyo imesema refa wa mechi hiyo Felix Brych hakukiuka taratibu
za mchezo wa soka nchini Ujerumani kufuatia maamuzi yake ya kuidhinisha
bao la mchezaji Stefan Kiessling lililofungwa katika dakika ya 72 baada
ya mpira aliopiga kwa njia ya kichwa kuingia langoni kupitia nje ya wavu
katika tundu na hivyo kuipa ushindi Leverkusen dhidi ya Hoffenheim ya
mabao mawili kwa moja.
Katika mechi zilizochezwa mwishoni mwa wiki, hakukuwa na mabadiliko katika kilele cha msamamo wa ligi baada ya Bayern
Munich, Borussia Dortmund na Bayer Leverkusen kushinda mechi zao.
Hata
hivyo hapo jana Hamburg iliendelea kupepea kwa kupata ushindi wa
mabao matatu kwa sifuri dhidi ya Freiburg chini ya kocha mpya Mholanzi
Bert van Marwjik.
Hamburg ambao sasa wametoka sare mara mbili na
kushinda mara mbili ili kusonga katika nafasi ya 12 chini ya kocha van
Marwjik, walisaidiwa sana na mlinda lango wa Freiburg Oliver Baumman,
aliyefanya makosa na kuwazawaidia magoli yote matatu.
Katika mechi nyingine, ya jana, Borussia Moenchengladbach walijikwamua
kutokana na kichapo cha wiki iliyopita mikononi mwa Hertha Berlin na
kuwakalifisha Eintracht Frankfurt mabao manne kwa moja na kusonga katika
nafasi ya nne kwenye ligi, baada ya ushindi wao wa tano katika mechi
zao tano za nyumbani msimu huu.
Jumamosi, Borussia Dortmund waliwazidi nguvu watani wao wa jadi
Schalke, kwa kuwarambisha magoli matatu kwa moja, wakati Bayern Munich
wakitokwa jasho na kuponyoka na ushindi wa mabao matatu kwa mawili dhidi
ya Hertha Berlin.
Bayer Leverkusen pia ilitoka nyuma na kuipiku
Augsburg mabao mawili kwa moja ili kubakia katika nafasi ya tatu kwenye
Bundesliga, ikiwa na pointi sawa na Dortmund, moja nyuma ya viongozi
Bayern.
Mainz iliwashinda washika mkia Eintracht Braunschweig 2-0, wakati nao
Hannover wakiwa na siku ngumu, walipofunzwa soka kwa kufungwa mabao
manne kwa moja nyumbani na Hoffenheim, mechi iliyojaa sarakasi chungu
nzima, na hata Hannover kumaliza mchezo ikiwa na wachezaji tisa
uwanjani.
Mchezaji Mame Biram Diouf alionyeshwa kadi ya njano kwa kudai penalty
katika dakika ya 10, na kisha Msenegal huyo akatimuliwa uwanjani baada
ya kupiga mbizi katika eneo la hatari.
Picha za video hata hivyo
zilionyesha kuwa ulikuwa uamuzi wa kujadiliwa. Naye Marcelo akaonyeshwa
kadi nyekundu katika kipindi cha pili kwa kulalamikia kwa hasira bao
lililofungwa la Hoffenheim. Wolfsburg iliishinda Werder Bremen magoli
matatu kwa sifuri.
No comments:
Post a Comment