Hii ni sehemu ya Hotuba ya Malinzi wakati akikabidhiwa ofisi.
“Tunakabiliwa na mashindano mbalimbali ya kimataifa. Mfano ni
mechi ya marudiano ya U/20 wanawake dhidi ya Msumbiji wiki ijayo,
Mitoano ya mashindano ya Afrika wanawake mapema mwakani, Mashindano ya
Chalenji Novemba mwaka huu, na mashindano ya kufuzu AFCON 2015. Yote
haya yanahitaji maandalizi ya haraka”.
Programu ya vijana.
“Ilani
yangu ya uchaguzi ilielezea azma ya Tanzania kuomba uenyeji wa fainali
za vijana za Afrika U/17 mwaka 2019. Jambo hili tutalizungumzia kwenye
kikao chetu cha utendaji leo. Ili tuwe na timu nzuri ya kucheza fainali
hizo tukiwa wenyeji hatuna budi mwaka kesho kuunda timu ya Taifa ya U/12
itakayokua pamoja kuelekea 2019. Programu yetu ya vijana tutakayoiandaa
sharti ijielekeze kwenye ratiba hii.”
Udhamini wa timu za vijana na za wanawake
“Hii
ni changamoto kubwa sana kwa TFF. Timu zetu za Taifa kuanzia zile za
wakubwa hadi za vijana ni brands, na kama ni brands inabidi ziingizwe
sokoni, ziuzwe kwa tunaodhamiria wawe wadhamini wa hizo timu. Kitengo
cha masoko lazima kiimarishwe ili kukabiliana na changamoto hizi.
Mdhamini ni mfanyabiashara, anapotoa pesa kudhamini brand fulani
anategemea matokeo mazuri kwake kwa njia ya kukuza biashara zake. Twende
kwa wadhamini tuwashawishi waone watafaidikia nini (leverage) kwa
kudhamini timu zetu. Tusisubiri waje tuwafuate sisi.”
Uwekezaji
“Jitihada
za haraka lazima zifanyike kuiongezea TFF uwezo wa kiuchumi. Ni muhimu
mtaalam mshauri (consultant) atafutwe atufanyie mchanganuo wa uwekezaji
katika ardhi yetu hii ya Karume ili tuwekeze kitega uchumi kama
ilivyokubaliwa kwenye mkutano mkuu. Aidha bidhaa zenye nembo yetu zianze
kuuzwa kwa utaratibu maalum ili shirikisho lipate haki yake.”
“Kabla
sijamaliza kuzungumza, niongelee suala la fujo viwanjani. Mpira ni
dakika tisini. Katika kipindi hicho uamuzi wa mwamuzi unakuwa ni wa
mwisho. Tusifiche upungufu wa timu zetu kwa kujificha nyuma ya kivuli
cha mwamuzi. Waamuzi wakionekana wamefanya makosa yawe ya makusudi au ya
bahati mbaya vyombo vya kuwahukumu vipo, mahakama ya waamuzi sio
mashabiki. Kitendo cha mashabiki kufanya fujo kabla, wakati na baada ya
mechi ya mpira kamwe hakikubaliki mahali popote duniani. Kanuni za
FIFA, CAF na TFF ziko wazi na adhabu zinajulikana. Moja ya adhabu hizi
ni timu husika kucheza kwenye uwanja mtupu usio na mashabiki kama
ilivyowatokea Al Ahly na Zamalek huko Misri au kucheza nje ya uwanja
wako kama ilivyowatokea Senegal ambao baada ya vurugu Dakar, Senegal
waliamriwa na FIFA mechi zao za nyumbani wachezee nje ya nchi na
wakachagua kuchezea Morocco.”
“Ndugu
zangu yaliyotokea majuzi Mbeya na Dar es salaam wote tumeyasikia na
wengine miongoni mwetu hapa ni mashuhuda. Ninasema iwe mara ya kwanza na
y a mwisho. Kwenye masuala ya kutekeleza mahitaji ya kanuni uongozi
wangu hautaionea haya klabu yoyote, iwe mpya au kongwe kwenye ligi yetu.
Ni jukumu la viongozi wa klabu kudhibiti wanachama na wapenzi wao.
Tabia ya benchi la ufundi kutoa matamshi yanayoweza kuamsha hisia za
mashabiki ni kinyume na taratibu na kanuni ziko wazi kuhusu jambo hili.
Viongozi wa klabu na mabenchi yao ya ufundi wakishindwa kutekeleza
wajibu wao tusilaumiane.”
“Ndugu
zangu ya kufanya ni mengi katika kuiendeleza soka yetu. Tunashukuru
Mungu kuwa uwezo wa kukabiliana na changamoto hizi tunao na tuna ari na
nia ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya mpira. Ombi langu kwenu
nyote ninaomba ushirikiano wa wadau wote kuanzia Serikali, Halmashauri,
mashirika ya umma na binafsi na NGO’s, nina imani tukishikamana
tutaifikia ndoto yetu ya kuing’arisha Tanzania kimpira kwenye anga za
dunia.”
No comments:
Post a Comment