Pengine sasa imeandikwa kwenye vitabu vya rekodi vya dunia kuwa, Li Na raia wa uchina amekuwa mtu wa kwanza kutoka barani Asia kunyakuwa taji la michuano ya wazi ya Australia ijulikanayo kama Australian Open kwa mchezaji mmoja mmoja.
Li Na ameweza kuingia kwenye kumbukumbu hiyo
muhimu baada ya mapema leo jumamosi kunyakuwa taji la pili ya Grand Slam ama
michuano yenye hadhi ya juu katika mchezo wa tenesi.
Alimfunga Mslovakia Dominika Cibulkova kwa seti tatu,ikiwa ni kwa pamoja 7-6 (7-3) 6-0.
Ikiwa ni fainali yake ya tatu ya michuano ya
Grand Slam baada ya kuingia kwenye fainal mbili na kushinda moja hapo
awali, sasa amekuwa mtu wa kwanza kutoka bara la Asia kucheza fainal
tatu na kunyakuwa ubingwa mara mbili.
Taji lake la kwanza la Grand Slam alishinda
mwaka 2011 kwenye michuano ya tenesi ya wazi ya Ufaransa maarufu kama
French Open, kisha akacheza fainal ya michuano ya Australian Open mwaka
jana ambapo aliingia fainal lakini akapoteza.
Sura yake iliishakuwa maarufu kwenye viwanja vya
Melbourne Park kunakofanyika michuano hiyo inayofikia tamati hapo
jumapili kwa fainali ya wanaume.
Akizungumza baada ya ushindi wake, Li alisema
"hatimaye nimelipata, fainali mbili zilizopita ilikuwa karibu sana
nishinde." Alisema Li Na mwenye umri wa miaka 31.
"Kwa sasa nashukuru jopo langu la ufundi, asante kwa wakala wangu kwa kunifanya kuwa tajiri,namshukuru sana. "
Aliongeza kwa kumshukuru mume wake ambaye
alikuwa kwenye jukwaa akimshuhudia, alimwambia " Asante sana, wewe ni
mume mwema. Pia una bahati."
Kwa upande mshindi wa pili wa michuano hiyo,
Cibulkova alisema anashukuru hii ni fainali yake ya kwanza katika michuano mikubwa
ya Grand Slam hivyo anashukuru jinsi alivyoweza kumudu mchezo huo.
Wachambuzi wa masuala ya tenisi wanabashiri
huenda Li Na akampiku gwiji wa Kimarekani Serena Williams kwenye viwango
vya ubora wa mchezo wa Tenesi duniani, hasa ikichagizwa na namna
ambavyo mwanadada huyo wa Kichina anavyoweza kumudu kucheza kwa juhudi
kubwa katika michezo yake mingi ya hivi karibuni.
Michuano inayofuata ya Grand Slam ya French Open huenda ikawa na mvuto zaidi na Li Na anapewa nafasi kubwa ya kufika fainali.
Li Na ni mchezaji wa tenesi kutoka Uchina ambaye
amekumbana na vikwazo vingi katika maisha yake ya uchezaji tenesi
ikiwemo kujigharamia mwenyewe kwenye michuano mbalimbali tangu alipotoka
kwenye timu ya taifa ya tenesi ya Uchina mwishoni mwa mwaka 2002 na
kisha kurejea tena mwaka 2004.
Ni mchezaji wa tenesi mwenye shahada ya Uandishi
wa Habari kutoka chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Huazhong
nchini Uchina.
No comments:
Post a Comment