Arsene Wenger ana nafasi ya kumnyamazisha Jose Mourinho Jumamosi timu
yake ya Arsenal itakapozuru Stamford Bridge ikilenga kupokonya Chelsea
udhibiti wa kinyang’anyiro cha kushinda Ligi ya Premia.
Hakuna njia bora zaidi ya kusherehekea mechi ya 1000 akiwa kwenye
usukani Arsenal kushinda kuvunja rekodi ya kutoshindwa nyumbani katika
ligi ambayo anajivunia mdosi huyo wa Chelsea ambaye mwezi uliopita
alipuuzilia mbali na kumtaja kuwa “mtaalamu wa kufeli”.
Vita vya maneno vimekuwa vikiendelea kwenye mbio za ligi ya premia
lakini ni uwanjani ambapo alama hushindwa na kupotezwa. Matokeo ya debi
hiyo ya Jumamosi huenda yakawa na umuhimu mkubwa kuamua nani atakwua
mshindi Mei 11.
Chelsea walionekana kudhibiti vyema mbio hizo hadi wikendi iliyopita
waliposhindwa 1-0 na Aston Villa.
Ushindi wa Liverpool, Arsenal na
Manchester City ulifanya mambo kuwa magumu zaidi kileleni.
Timu hiyo ya Mourinho bado ina uongozi katika msimamo wa ligi ikiwa na alama nne mbele ya Arsenal
na Liverpool, ingawa wote wawili wana mechi moja ambayo hawajacheza,
huku City walio alama sita nyuma ya Chelsea wakiwa na mechi tatu za
kucheza.
City watakuwa nyumbani kukabiliana na klabu ya Fulham inayoshika mkia
katika ligi Jumamosi, huku Liverpool wakisaka ushindi wao wa sita mfululizo
ugenini kwa Cardiff City ambao wanapigana kukwepa shoka la kushushwa daraja.
Wenger alitaja matamshi ya Mourinho kuwa ya “kijinga” na ya “kukosa
heshima” mwezi jana baada ya kocha huyo Mreno kufanyia mzaha ukame wa
mataji wa misimu minane wa Mfaransa huyo.
"Ninaogopa kufeli? Yeye ni mtaalamu katika kufeli. Mimi hapana. Kwa
hivyo mtu akidhani kwamba hajakosea, na kwamba naogopa kushindwa, ni kwa
sababu huwa sishindwi mara nyingi,” akasema Mourinho.
Wenger alikuwa ameanzisha majibizano hayo alipouliza maswali kuhusu
nia ya Mourinho kusema timu yake ni “farasi mdogo” kwenye mbio dhidi ya
Manchester City ambao ni "jaguar".
Arsenal walionekana kuteleza baada ya kushindwa mara mbili mfululizo
katika ligi, lakini ushindi wa 1-0 dhidi ya wapinzani wao kutoka London
kaskazini Tottenham Hotspur wikendi iliyopita ulifufua matumaini yao ya
kushinda taji hilo mara ya kwanza tangu 2004 – mwaka ambao Mourinho
alifika mara ya kwanza London akijiita “the Special One” yaani Yule
Mteule.
Ushindi Stamford Bridge, ambapo Mourinho hajawahi kupoteza mechi ya
ligi, utawaweka alama moja kutoka kileleni wakiwa na mechi moja ambayo
hawajacheza, jambo ambalo litakuwa kibarua ikizingatiwa kwamba Jack
Wilshere, Aaron Ramsey, Theo Walcott na Mesut Ozil wanauguza majeraha.
No comments:
Post a Comment