Real Madrid wamepewa fursa ya kulipiza kisasi kichapo walichopewa na
Borussia Dortmund msimu uliopita katika nusu fainali ya UEFA Champions
League. Timu hizo mbili zimepangwa tena katika robo fainali
Mabingwa watetezi wa taji la vilabu bingwa Ulaya Bayern Munich wamepangwa na Manchester United, mchezo ambao utarejesha kumbukumbu za fainali yao ya mwaka wa 1999 wakati United
ilifunga magoli mawili katika dakika za mwisho mwisho na kupata ushindi
wa mabao mawili kwa moja. Paris St Germain watakabana koo na Chelsea
wakati Barcelona na Atletico Madrid zote kutoka uhispania zikishuka
dimbani katika mpambano unaotarajiwa kuwa mkali.
Mshambuliaji wa BVB Mpoland Robert Lewandowski, aliyefunga magoli yote
manne katika ushindi wa Dortmund wa mabao manne kwa moja dhidi ya Real
Madrid msimu uliopita, atakuwa nje katika mechi ya kwanza dhidi ya
mabingwa hao mara tisa wa ulaya ili kutumikia adhabu ya kadi nyingi za
njano..
Afisa Mkuu mtendaji wa BVB Hans-Joachim Watzke alisema baada ya
Lewandowski kupewa kadi ya njano katika mechi y amkondo wa pili dhidi ya
Zenit St Petersburg kuwa “hilo ni pigo kubwa. Yeye ni mchezaji mzuri.
Ulikuwa uamuzi wa kushangaza”.
Amesema Real ni kikosi kikali lakini watajitahidi kila wawezavyo kwa
sababu katika awamu hii hakuna timu yoyote dhaifu. Bayern nao ambao
wanalenga kutwaa mataji ya Champions League, Bundesliga na Kombe la
Shirikisho, kwa msimu wa pili mfululizo, wameahidi kuwa hawatawadharau
Manchester United licha ya matatizo ya klabu hiyo ya Uingereza katika
ligi ya nyumbani.
Paris St Germain watalenga kujipiga kifua kama miamba wa Ulaya
watakapokutana na Chelsea. Timu hizo mbili zimepangwa pamoja mara moja
tu mnamo mwaka wa 2004 katika awamu ya makundi ya Champions League.
Chelsea ilishinda mjini Paris kabla ya kutekwa sare mjini London. Mechi
za mkondo wa kwanza zitachezwa mnamo Aprili mosi na mbili huku mikondo
ya pili ikichezwa April inane na tisa. Finali itakuwa mjini Lisbon mnamo
Mei 24.
No comments:
Post a Comment