Hamburg iliponea chupuchupu na kujiondoa katika kundi la timu tatu
zinazoshika mkia kwa mara ya kwanza tangu Januari baada ya kusajili
ushindi wa magoli mawili kwa moja nyumbani dhidi ya washika mkia
Nuremberg.
Huku Hamburg ikifanya kila iwezalo kuepuka shoka la kushushwa daraja,
Mirko Slomka aliyechukua usukani kutoka kwa Bert van Marwijk kama kocha
mwezi uliopita ameisaidia timu yake kusonga hadi nafasi ya 14.
Nuremberg wameshuka hadi nafasi ya 15 wakati VfB Stuttgart, waliotoka
sare ya goli moja kwa moja na Werder Bremen siku ya Jumamosi chini ya
mkufunzi Huub Stevens wakijikuta katika nafasi ya pili kutoka nyuma.
Freiburg walisonga hadi nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi
lakini bado wako katika kiticho cha kushushwa ngazi, licha ya kusajili
ushindi wa mabao manne kwa moja dhidi ya Eintracht Frankfurt hapo jana.
Kileleni mwa ligi, viongozi Bayern Munich wanaweza kutawazwa mabingwa wa
msimu huu Jumamosi ijayo, huku kukiwa na mechi nane msimu kukamilika.
Hii ni baada ya ushindi wao wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Bayer
Leverkusen kuwapa uongozi wa pengo la pointi 23.
Miamba hao wa Ulaya
Beyern huenda wakapewa uchampioni kwa mara ya 24 kama watawabwaga Mainz endapo mahasimu wao Borussia Dortmund na Schalke wote watoke sare.
Kiungo wa
Bayern Bastian Schweinsteiger ni mmoja wa waliotikisa wavu.
"Bila
shaka kila kitu hakikwenda sawa, kwa sababu Leverkusen walikuwa
wasumbufu sana.
ulikuwa mchezo mgumu. Wakati mwingine unapaswa kuwa na
uvumilivu kidogo. Labda haikuwa jioni nzuri ya kabumbu, lakini
tulishinda mechi na hilo ndio jambo muhimu kabisa".
Leverkusen wako katika nafasi ya nne nyuma ya Schalke ambao waliwaadhibu
Augbsurg mabao mawili kwa moja siku ya Ijumaa. Borussia Dortmund
waliduwazwa kwa kichapo cha mabao mawili kwa moja na Borussia
Moenchegladbach mapema Jumamosi.
Dortmund sasa wako pointi moja mbele ya
nambari tatu Schalke kabla ya mchuano wao wa utani wa Bonde la Ruhr
mnamo Machi 25.
Kocha wa Gladbach Lucien Favre aliurefusha mkataba wake wiki
iliyopita hadi mwaka wa 2017 na timu yake ilionyesha mchezo wa hali ya
juu katika kipindi cha kwanza na kufunga magoli mawili katika dakika
tisa.
Huyu hapa kocha Lucien Favre.
"Hatimaye tuna ushindi. Ulikuwa
wakati mgumu. Ni wazi sote tumeridhika. Walitufanya kucheza kwenye
mstari wa katikati. Walikuwa hatari sana kwa kuung'ang'ania mpira na
kufanya mashambulizi ya kasi. Wakati mwingine tulizidiwa, tunahitaji
kusema wazi, lakini tuliweza kupata mabao kwa wakati uliofaa".
FC Mainz ilisonga hadi nafasi ya tano baada ya kusajili ushindi mnono wa
mabao manne kwa mawili dhidi ya Hoffenheim. Kocha wa Hoffenheim Martin
Gisdol alisalia kujikuna kichwa tu baada ya kichapo hicho.
"Ni vigumu
kuelezea….Unapompa mpinzani magoli ya wazi. Tunapaswa kujilaumu sisi
wenyewe kwa makosa yetu kutokana na mchezo mzuri tuliokuwa nao.
Tungebidi kuwa mbele magoli hata matano kwa sifuri. Lakini tukafunga
mbili tu….na katika Bundesliga hicho ni kishindo".
Mainz sasa wanaendelea kuwinda nafasi ya kucheza katika jukwaa la ulaya
msimu ujao na wanapungukiwa na points tatu tu wakipata kibali cha
kugaragaza soka la Champions League.
Wolfsburg wamedondoka hadi nafasi
ya sita baada ya sare ya goli moja kwa moja na washika mkia Eintracht
Braunschweig. Matarijio ya Hertha Berlin kucheza Ulaya yaligonga mwamba
baada ya kushindwa nyumbani mabao mawili bila jawabu mikononi mwa
Hanover 96 na hivyo kusalia katika nafasi ya tisa.
No comments:
Post a Comment