KWA MAWASILIANO ZAIDI TUMIA BARUA PEPE rockersports212@yahoo.com AU TUPIGIE KUPITIA NAMBARI 0767166607 AU 0717166607. KARIBU SANA. 66666666607 AU 0717166607

Sunday, October 19, 2014

Tahadhari Yanga: Nani wa kumwambia Maximo juu ya upangaji wa kikosi chake? Jahazi linazama na abiri wanaona

Mchezo huu kabla ya kuanza ulikuwa na picha ya Yanga kuwa na kikosi kizuri zaidi ukilinganisha na Simba ambayo haikuwa na wachezaji wengi wazoefu huku Simba langoni ikilindwa na Manyika Peter (Manyika Junior) akisaidiwa na walinzi wa kati Hassan Isihaka na Josefu Owino.
Pembeni Simba inayofundishwa na kocha Patrick Phiri ilikuwa na Mohamed Hussein (Shabalala) na Willian Galas na kiungo wa chini Jonas Mkude na Saidi Ndemla huku washambuliaji wakiwa ni Amri Kiemba, Haruna Chanongo, Elias Maguri na Emmanuel Okwi.
Baadaye aliingia Shabani Kisiga (Malon) na Ramadhani Singano(Messi) kuchukua nafasi za Said Ndemla na Jonas Mkude aliyeumia bega. 
Yanga golini alikuwepo Deogratius Munishi(Dida) kulia Juma Abdul na kushoto ni Oska Joshua.
Katikati sehemu ya ulinzi ni Kelvin Yondani na nahodha Nadir Haroub (Canavaro) huku kiungo kikiongozwa na Mbuyu Twite na Hassan Dilunga pembeni Andrey Coutinho na Mrisho Ngasa na washambuliaji wa kati ni Gerson Santos Jaja na Haruna Niyonzima.
Baadaye aliingia Simon Msuva kuchukua nafasi ya Haruna Niyonzima na Hamisi Kiiza aliyechukua nafasi ya Jaja.
Uzoefu kwa wachezaji wa Yanga ukilinganisha na kikosi cha Simba haikuwa dawa ya kuisaidia timu hiyo kuibuka na ushindi jambo ambalo limezua maswali ya nini kinaisibu Yanga inapokutana na Simba hususani katika miaka miwili iliyopita.
Mbinu anazotumia kocha wa Yanga mbrazil Macio Maximo zinaonekana hazina mashiko katika kutoa matokeo ya ushindi jambo ambalo wakati mwingine inadhaniwa kuwa ni aina ya upangaji wake wa kikosi ambapo amekuwa akimtumia Coutinho ambaye anaonekana hana madhara sana kutokana na kukosa nguvu huku Jaja akiwa na uwezo mdogo wa kutafuta mipira kwa uwezo wake zaidi akisubiri mipira huru na kuvizia au atengewa ali aweze kupiga akiwa huru.
Maximo sasa inabidi aanze kuwaamini washambuliaji wake wengine kama vile Gerson Tegete, Hussein Javu na Said Bahanuzi ambao wanaonekana kupoteza matumaini ya kucheza tena ndani ya kikosi cha Yanga si tu katika michezo ya ligi hata ile ya kimataifa hususani katika michuano ya vilabu kombe la shirikisho timu hiyo ikiwa ni wawakilishi wa Tanzania.
Swali ni nani wa kumwambia Maximo wakati jahazi likizama na abiria wakiona? bila shaka ni wasaidizi wake Leonardo Neiva, Salvatory Agustino Edward na Shadrack Nsajigwa. .
Iko wazi katika mchezo mgumu kama wa Yanga na Simba kocha anapaswa kuongeza umakini ili kulinda heshima ya vilabu hivi ambavyo vimewagawa watanzania katika makundi mawili ya ushabiki. Si kwa kutikisa masikio wala kung'ata maneno Maximo ambaye aliwahi kuwa kocha wa timu ya taifa anapaswa kujua kuwa heshima yake italindwa mbele ya wanachama na wapenzi wa Yanga kwa matokeo mazuri ya uwanjani na si vinginevyo.
Katika mchezo wa jana ilikuwa rahisi kwake kuanza kuonyesha kweli anataka kulinda heshima yake kwa kumtumia mchezaji kama Simon Msuva tangu mapema huku uzoefu wa Nizar Khalfani uzoefu wake ukihitajika sana kama ilivyo kwa Tegete, Husseni Javu na Hamisi Kiiza.
Sina maana kuwa Simba walikuwa na kikosi kibaya, uwezo wa Simba katika mchezo huo ulitokana na mapungufu yaliyo onyeshwa na Yanga na ndio maana Simba walitawala mchezo katika sehemu kubwa ya mchezo katika kipindi cha kwanza.
Amri Kiemba na Shabani (Kisiga Malon)   walikuwa ni nguzo baada ya kuondoka kwa Mkude aliyeumia. Endapo Elias Maguri na Okwi wangepata nafasi zaidi za kulenga lango 'shoot on target' Yanga wangelala mapema.
Hongera kwa Hassan Isihaka na Mohamed Hussein Shabalala wanaonekana kuanza kukomaa vizuri huku pia mlinda mlango namba tatu wa Simba Manyika Peter akionyesha uwezo kwa kutumia utulivu langoni, kiasi pengo la wazoefu Hussein Sharif (Cassilas)  na Ivo mapunda kutokuonekana.
Ninachotaka kusema hapa ni kocha wa Yanga kama ataendelea kuipanga safu yake ya ushambuliaji kwa kubahatisha  basi unaweza kuwa msimu mgumu kwa klabu hiyo kongwe hapa nchini.

No comments:

Post a Comment