MAANDALIZI ya Mkutano Mkuu wa Chama cha Waandishi wa
Habari za Michezo Tanzania (TASWA) yanaenda vizuri na wajumbe wanatarajiwa
kufika Bagamoyo Ijumaa Desemba 28, 2012 mchana kwenye hoteli ya Kiromo View
Resort watakapolala na kufanyia mkutano.
Ijumaa hiyo washiriki watatembelea maeneo mbalimbali ya
kihistoria Bagamoyo na jioni kutakuwa na mechi ya kirafiki kati ya timu ya soka
ya TASWA FC na Bagamoyo Veterani itakayofanyika Uwanja wa Mwanakalenge na usiku
wajumbe watakuwa na chakula cha pamoja na kubadilishana mawazo kuhusiana na
masuala mbalimbali yahusiyo michezo na taaluma ya habari.
Mkutano Mkuu utafunguliwa Jumamosi Desemba 29, saa tatu
asubuhi na mgeni rasmi atakuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kusaidia timu za Taifa
za Vijana, Ridhiwani Kikwete.TASWA imechukua jukumu la kumualika kutokana na
kuwa mdau mkubwa na rafiki wa chama chetu.
Mkutano utafungwa jioni ya siku hiyo na Mkurugenzi wa
Idara ya Habari (MAELEZO), Assah Mwambene ambaye hiyo pia itakuwa nafasi nzuri
kwake kuweza kuzungumza na wana habari kuhusiana na masuala mbalimbali ya
kitaaluma.
Katika
mkutano huo wanachama wa TASWA watapata fursa ya kupokea na kujadili Ripoti ya
Utendaji ya chama, Mapato na Matumizi, maendeleo ya chama na masuala mbalimbali
yanayohusu waandishi wa habari za michezo na maendeleo ya michezo kwa ujumla
Pia
kutakuwa na semina maalum itakayoendeshwa kwa washiriki wa mkutano huo, ili
wawe na uelewa kuhusiana na ajenda ya kuinua kipato kwa wanachama ambayo nayo
itajadiliwa kwenye mkutano huo.
Kamati ya
Utendaji ya TASWA imekubaliana iwasaidie wanachama wake waweze kujitegemea kwa
kuanzisha Chama cha Akiba na Mikopo (SACCO’S), lakini imeamua kwanza iwaite
wataalamu wa vyama vya ushirika watoe elimu juu ya jambo hilo na kukishakuwa na
uelewa wa kutosha suala hilo litakuwa kama ajenda kamili ya kuanzisha chama
hicho kwenye mkutano wetu.
No comments:
Post a Comment