TRA YAIDAI YANGA MIL. 203 ZA PAYE, SIMBA MIL 50.7
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema inazidai klabu za Simba na
Yanga jumla ya sh. milioni 253.7 kutokana na kukwepa kulipa kodi ya Lipa
Kama Unavyopata (PAYE).
Kiasi hicho cha fedha ni makato ya PAYE kwa ajili ya wachezaji wa kigeni
waliosajiliwa na klabu hizo mbili kwa nyakati tofauti, na ambao kwa
muda mrefu walikuwa hawakatwi kodi kulingana na sheria za kodi nchini.
Kaimu Mkurugenzi wa Elimu kwa Walipakodi wa TRA, Hamis Lupenja alisema
mjini Dar es Salaam jana kuwa, mamlaka hiyo inaidai Yanga sh. milioni
203 na tayari imekwishafunga akaunti yake ya benki ya CRDB.
Lupenja alisema Simba inadaiwa sh. milioni 50.7, lakini akaunti ya klabu
hiyo bado haijafungwa na wametoa muda kwa viongozi wake kulipa deni
hilo kabla ya hatua ya kufungiwa kuchukuliwa.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema TRA imekuwa ikizikumbusha mara kwa mara
klabu hizo kongwe nchini kuhusu umuhimu wa kulipa kodi ikiwa ni pamoja
na kutoa elimu.
Alisema hatua ya kuzifungia klabu inakuja baada ya klabu kushindwa
kutekeleza wajibu wake na kuongeza kuwa, iwapo klabu hizo zitashindwa
kulipa fedha hizo, hatua itakayofuata ni kukamata mali za klabu.
Lupenja alisema zoezi hilo halitaishia kwa klabu za Simba na Yanga,
badala yake litafanyika kwa zote, ambazo zimewahi kusajili wachezaji wa
kigeni.
"Unajua kwa muda mrefu klabu zetu zimekuwa zikileta wachezaji wa kigeni,
lakini hawakatwi kodi na deni linakuwa kubwa, hivyo kwa sasa tumeamua
kufuatilia kwa kina na tulianza na baba yao Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), na sasa watoto ambao ni klabu," alisema Lupenja.
Alisema lengo la TRA siyo kudidimiza michezo, bali ni kutekeleza wajibu
wa kukumbusha watu wote umuhimu wa kulipa kodi.
Mwishoni mwa mwaka jana, TRA ilifunga akaunti ya TFF baada ya shirikisho
hilo kudaiwa sh. milioni 157,407.968 zilizotokana na malimbikizo ya
PAYE za makocha wa kigeni wa timu za Taifa.
Hata hivyo, akaunti hiyo ilifunguliwa baada ya mazungumzo kati ya TRA,
TFF na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa vile fedha
hizo zimetolewa na wadhamini, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom kwa
ajili ya klabu za ligi kuu.
Alipoulizwa kuhusu hatua, ambazo Yanga imechukua baada ya akaunti yao
kufungwa, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Lawrence Mwalusako alikiri kuwa ni
kweli akaunti hiyo imefungwa na wameathirika.
Mwalusako alisema akaunti hiyo ndiyo inayopokea fedha za malipo ya kadi
za wanachama kabla ya kushiriki katika mkutano mkuu wa klabu hiyo
utakaofanyika Januari 19 mwaka huu.
Hata hivyo, Mwalusako alisema uongozi wa klabu yake unaendelea
kulishughulikia suala hilo na huenda likatatuliwa hivi karibuni. Hakuwa
tayari kutaja hatua wanazotarajia kuchukua.
Viongozi wa Simba hawakuweza kupatikana jana kuzungumzia suala hilo kwa
vile kila walipopigiwa simu, hawakuwa tayari kuzipikea.
No comments:
Post a Comment