KWA MAWASILIANO ZAIDI TUMIA BARUA PEPE rockersports212@yahoo.com AU TUPIGIE KUPITIA NAMBARI 0767166607 AU 0717166607. KARIBU SANA. 66666666607 AU 0717166607

Monday, January 7, 2013

UTATA KAMBI YA TIMU YA TAIFA WACHEZAJI 6 TU NDIO WALIORIPOTI.

 Wakati kambi ya timu ya taifa ikiingia siku yake ya pili hii leo kwa ajili ya maandalizi ya michezo kadhaa ya kirafiki ya kimataifa, taarifa zinasema ni wachezaji 6 tu ndio walioripoti kambini mpaka kufikia jioni ya leo.

Akiongea na Rockersports kocha msaidizi wa timu hiyi Sylvester Mashi amesema hali hiyo imetokana na wachezaji wengi kuendelea kuwepo katika timu zao ambazo zimekuwa na majukumu mbalimbali ikiwa ni pamoja na Yanga yenye wachezaji 5 wa timu ya taifa ambao bado wako nchini Uturuki wakiendelea na kambi ya wiki mbili.

Kwa upande wa wachezaji wa Simba wao bado wanaendelea na michuano ya kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar ambapo Mashi amesema wanategemea kuwapata wachezaji hao usiku wa leo na kufanya idadi ya wachezaji 12 idadi ambayo itawawezesha kuanza mazoezi hapo kesho.
 Kwa upande wa wachezaji wa Azam fc Mashi amesema wanategemea kuwapata hapo kesho kwani wanasubiri mchezo wao wa leo wa michuano ya kombe la Mapinduzi.

Kuhusu wachezaji wa Yanga Mashi amesema shirikisho la soka nchini TFF linaendelea na mchakato wa kuwapata wachezaji hao mapema na kwamba wanaimani kuwa wachezaji wa timu ya taifa walioko katika kambi ya Yanga watawahi safari ya Afrika kusini.

 Taifa stars inawachezaji 5 kutoka Yanga ambao ni Kelvin Yondan, Frank Domayo, Athumani Iddi Chuji, Simon Msuva na Nadir Haroub Kanavaro.
Kutoka Simba ni Amir Maftaha, Mwinyi Kazimoto, Juma Kaseja, Shomari Kapombe na Amri Kiemba.
Kutoka Azam fc ni Erasto Nyoni, Salum Abubakar, Khamis Mcha, Aggrey Moris, Aishi Manula na John Bocco. 

Wachezaji ambao wamesha ripoti kambini ni pamoja na Juma Kaseja , Issa Rashid, Aggrey Morris, Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu na Mrisho Ngasa.

Taifa Stars inataraji kuelekea nchini Ethiopia kwa mchezo wa kimataifa wa kirafiki tarehe 11/01/2013 dhidi ya wawakilishi hao wa kanda ya Afrika mashariki na kati katika fainali za mataifa ya Afrika.   
 Kwa vyovyote vile inaonekana kuna uwezekano mdogo wa kambi hiyo ya timu ya Taifa kuwapata wachezaji wa Yanga ambao programu yao mazoezi ya wiki mbili itakamilika mwishoni mwa juma hili. 
 
Kwa upande wa Simba nao wanajipanga kwa safari ya kuelekea nchini Oman kwa kambi ya maandalizi ya ligi kama ilivyo kwa Yanga ambao wanaendelea na kambi hiyo nchini Uturuki ambapo bila shaka watahitaji kuelekea huko na wachezaji wao wote.

Aidha kwa upande wa Azam yenye dhamira ya kutetea taji lao la kombe la mapinduzi hivi sasa wanaendelea vema na michuano hiyo ambapo nao watataka kuendelea kuwatumia wachezaji wao mpaka fainali endapo watapata nafasi ya kufika katika hatua hiyo ya michuano hiyo.

Hata hivyo kocha msaidizi Mashi anaamini kwa jitihada za TFF watafanikiwa kuwapata wachezaji wote waliotajwa na kocha mkuu wa timu ya taifa Kim Poulsen na kufanikisha programu ya timu ya Taifa ikiwa ni pamoja na kufanikisha safari hiyo ya nchini Ethiopia.

Stars inajiwinda na mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia dhidi ya Morocco mchezo ambao utapigwa mwezi machi.

No comments:

Post a Comment