Timu ya Young Africans Sports Club
imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya timu ya Arminia Bielefeld ya Ujerumani
katika mchezo wa kirafiki uliofanyika leo jioni katika uwanja wa Adora
Football pembeni kidogo ya mji wa Antalya.
Armini Bielefeld ilianza soka kwa kasi kwa lengo la kujipatia bao la
mapema lakini umakini wa walinzi wa Yanga na mlinda mlango Ally Mustafa
'Barthez' ilikuwa kikwazo kwao kwani mashambulizi yao yaliishia mikononi
mwake.
Ikiwa ni mchezo wake wa kwanza wa kujipima nguvu Young
African iliweza kuonyesha soka safi katika kipindi cha kwanza hali
iliyowashangaza wajerumani hao na kipindi cha pili kuamua kufanya
mabadiliko ya kikosi kizima.
Viungo wa Yanga Frank Domayo, Haruna
Niyonzima na Kabange Twite waliweza kutawala mchezo kwa dakika 45 zote
za kipindi cha kwanza huku baadhi ya wajerumani waliokuwa wakishuhudia
mchezo huo kushangazwa na kiwango cha timu ya Yanga
Hadi mapumziko timu zote zilikwenda mapumziko , Young Africans 0 - Arminia Bielefeld.
Kipindi
cha pili Arminia Bielefeld iliamua kubadilisha kikosi chake chote cha
wachezaji kwa lengo la kuingiza nguvu mpya ili waweze kuikabili kasi ya
wachezaji wa Yanga ambao walionekana kuwa imara na bora zaidi.
Dakika
ya 55 Yanga ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Said Bahanuzi na David
Luhende na nafasi zao kuchukuliwa na Jerson Tegete na Saimon Msuva.
Jerson
Tegete aliipatia Young Africans bao la kwanza dakika ya 60 ya mchezo,
akiunganisha pasi safi aliypewa na Saimon Msuva aliyewatoka walinzi wa
Arminia Bielefeld na kumpa pasi Tegete ambaye aliukwamisha mpira wavuni
na kuhesabu bao la kwanza.
Kuona hivyo wajerumani walikuja juu
kusaka bao la kusawazisha, lakini bado ukuta wa Yanga uliendelea
kuonekana kuwa makini lakini makosa ya mshika kibendera yaliipelekea
Armini Bielefeld kupata bao la kusawazsiha dakika ya 81 kupitia kwa Eric
Agyemang ambaye alikua ameotea.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika Young Africans 1 - 1 Armini Bielefeld.
Kocha
Mkuu wa Young Africans Ernest Brandts amesema amefurahishwa na kiwango
walichokionyesha wachezaji wake na anaamini kadri siku zinavyokwenda
wanazidi kuimarika na kuwa bora, hivyo katika michezo mingine
wataendelea kuonyesha mabadiliko makubwa.
Young Africans:
Ally Mustafa 'Barthez, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub
'Cannavaro', Kelvin Yondani, Kabange Twite, Haruna Niyonzima/Nizar
Khalfan, Frank Domayo/Nurdin Bakari, Said Bahanuzi/Jerson Tegete, Didier
Kavumbagu, David Luhende/Saimon Msuva
No comments:
Post a Comment