BONANZA la vyombo mbalimbali vya habari
lililopangwa kufanyika Aprili 6 mwaka huu viwanja vya Leaders Klabu
likiandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), sasa
litafanyika viwanja vya Sigara (TCC), Chang’ombe pia Dar es Salaam.
Uamuzi
wa kuhamisha bonanza hilo umechukuliwa na sekretarieti ya TASWA kutokana na
maombi ya waandishi wengi wa michezo kwa vile siku hiyo kuna mechi ya Kombe la
Shirikisho la Soka Afrika kati ya timu ya soka ya Azam na Barrack Young
Controllers ya Liberia itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam siku
hiyo.
Azam ni
timu pekee ya Tanzania iliyobaki kwenye michuano ya Afrika kwa ngazi ya klabu
baada ya Simba na Jamhuri ya Pemba kutolewa katika raundi ya awali.
Tunaamini
kwa bonanza kufanyika Sigara itakuwa rahisi kwa wadau wetu kushiriki kwenye
bonanza na wale wengine watakaohitaji kwenda uwanjani wafanye hivyo wakitokea
Sigara kwa hakuna umbali mrefu na kisha warejee kujumuika na wenzao mpaka
mwisho.
Tunawaomba
radhi kwa mabadiliko hayo, lakini yakiwa na lengo la kujenga na kuwa pamoja na
wenzetu wa Azam kuhakikisha tunashirikiana nao kwa namna mbalimbali siku hiyo.
Bonanza
hili linadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) likiwa na lengo la kuwaweka
pamoja waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa, michezo, uchumi, afya
na mambo mengine pamoja na wafanyakazi wa vyombo mbalimbali vya habari ili
kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja.
Bonanza
hilo ambalo litahusisha wadau 1,500 kutoka vyombo mbalimbali vya habari
litaambatana na michezo mbalimbali itakayohusisha vyombo vyote vitakavyoshiriki
na pia kutakuwa na burudani ya muziki kutoka katika moja ya bendi kubwa za
muziki wa dansi hapa nchini, ambayo itatangazwa siku zijazo.
No comments:
Post a Comment