Frank Ribery( kulia) |
Vilabu vinavyoshiriki ligi ya Ujerumani Bundesliga ambayo
iko mapumzikoni hivi sasa vimeanza rasmi kambi ya mazoezi wiki hii.
Mabingwa wa Bundesliga Bayern Munich na Schalke 04 wako nchini Dubai ,
makamu bingwa Borussia Dortmund wanaanza kambi nchini Uhispania wiki
ijayo na Bayer Leverkusen halikadhalika wako nchini Uhispania.
Lakini wakati taarifa hizo zikiarifu vivyo, ni kwamba mshambuliaji wa pembeni wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ufaransa
Frank Ribery wakati huo huo ameteuliwa kuwa mchezaji bora wa nusu
ya kwanza ya ligi ya Ujerumani Bundesliga uteuzi uliofanywa na wachezaji wenzake wa ligi
hiyo.
Arjen Robben pia wa Bayern ameshika nafasi ya pili wakati Marco
Reus wa Borussia Dortmund ameshika nafasi ya tatu.
Ligi nyingine Ulaya
Ligi za mataifa mengine hata hivyo zinaendelea , ambapo hapo jana
Juventus Turin ilitunisha misuli yake dhidi ya Roma na kuirarua kwa
mabao 3-0. Kabla ya hapo Fiorentina iliibuka kidedea kwa ushindi wa bao
1-0 dhidi ya Livorno.
Matukio mengine
1)Matumaini ya mshambuliaji wa Italia Giuseppe Rossi
kucheza katika kombe la dunia huenda yakatatizwa baada ya mchezaji huyo
wa Fiorentina kupata maumivu katika goti lake la mguu wa kulia ambalo
limekuwa na matatizo kila mara katika mchezo wa jana Jumapili dhidi ya
Livorno.
2)Gareth Bale amepona maumivu katika mguu wake wa kushoto
na atakuwamo katika kikosi cha Real Madrid ambacho kitashuka dimbani leo
jioni kupambana na Celta Vigo.
3)Katika michezo ya jana Jumapili katika ligi ya Uhispania la Liga
Barcelona iliirarua Elche kwa kuipa kipigo cha mabao 4-0. Ushindi huo wa
Barca hata hivyo umekuja bila ya mshambuliaji wake hatari Lionel Messi.
Kocha wa Barcelona Gerardo Tata Martino amesisitiza hata hivyo kuwa
hatamharakisha Messi kurejea uwanjani katika pambano la wababe walioko
kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo dhidi ya Atletico Madrid mwishoni mwa
juma lijalo. Messi hajacheza tangu alipoumia misuli katika mchezo dhidi
ya Real Betis mapema mwezi Nivemba na alikuwa mtazamaji tu wakati
mabingwa hao waliporejea kileleni mwa msimamo wa ligi jana katika
ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Elche.
4)Manchester United itaangalia majaliwa yake katika kombe la ligi ili
kurejesha imani kwa mashabiki katika msimu huu wakati watakapokuwa
wageni wa Sunderland kesho Jumanne katika mchezo wa kwanza katika nusu
fainali.
Jana Jumapili Manchester United iliangukia pua pale ilipoyaaga
mashindano ya mwaka huu ya kombe la FA baada ya kuzabwa mabao 2-1 dhidi
ya Swansea City katika uwanja wa nyumbani wa Theather of Dreams , Old
Trafford.
Licha ya kuwa United bado inaendelea kucheza katika harusi mbili , ligi
ya mabingwa wa Ulaya Champions League na kombe la ligi, kombe hilo ndio
matumaini yao makubwa kuweza kuokoa msimu ambao unaonekana kuwa wa
maafa.
Wakati kocha wa zamani wa Manchester United Sir Alex Ferguson hatimaye
alipobwaga manyanga katika kazi ya kuifunza timu hiyo alisimama katika
nyasi za Old Trafford na kuwatafadhalisha mashabiki wa Man United kumpa
ushirikiano na kumuunga mkono mrithi wake aliyemteua David Moyes kwa
kukumbuka nyakati mbaya pamoja na zile nzuri.
Lakini baada ya jana Manchester United kunyofolewa kutoka katika
kinyang'anyiro hicho cha kombe la FA mashabiki hawakusita kuonesha
kufadhaika kwao.
Chelsea wamepangwa dhidi ya Stoke City katika kombe hilo la FA katika
duru ya nne katika upangaji wa mchezo hiyo jana Jumapili. Liverpool
ambayo iliiangusha Oldham Athletic kwa mabao 2-0 jana itawatembelea
Bournermouth ama Burton Albion. Zawadi ya Swasea City kwa kuwaondoa
Manchester United katika kinyang'anyiro hicho itakuwa ziara kwa
Birmingham City , Bristol Rovers ama Crawley Town.
No comments:
Post a Comment