Constantine anatazamiwa kufanya mazungumzo na shirikisho hilo la Ferwafa Alhamisi. |
Timu taifa ya soka ya Rwanda inamtaka Raia Muingereza Stephen Constantine kuwa mkufunzi wake katika mkataba wa miaka miwili.
Tayari shirikisho la soka nchini humo limempendekezea mkataba wa miaka miwili.
Shirikisho la kandanda la taifa hilo
linamtaka mkufunzi atakayechukua usukani baada ya Eric Nshiyamana,
ambaye mkataba wake na timu hiyo utatamatika tarehe 31 mwezi Julai.
Kocha huyo wa zamani wa Millwall mwenye umri wa
miaka 51, ana uzoefu wa kandanda ya bara la Afrika, hasa ikizingatiwa
kuwa alikuwa mkufunzi wa timu ya taifa ya Malawi tangia mwezi Februari
mwaka wa 2007 hadi Aprili mwaka wa 2008.
Constantine anatazamiwa kufanya mazungumzo na shirikisho hilo la Ferwafa Alhamisi.
Msemaji wa Shirikisho la Soka la Rwanda bwana Vedaste Kayiranga aliiambia BBC kwamba makubaliano yalikuwa yamefikiwa.
Kocha wa zamani wa Ghana Ratomir Djukovic, kocha
wa Botwana Peter Butler na kocha wa zamani wa Tanzania Kim Poulsen
walikuwa miongoni mwa waliotarajia kupewa kazi hiyo lakini Kayiranga
alisema kuwa walipendezwa na Constantine, na kwamba alikuwa tayari
kujiunga na timu hiyo ya taifa la Rwanda.
Constantine aliye na leseni kutoka kwenye
shirikisho la soka ulimwenguni majuzi aliisaidia Nea Salamis kutoka
katika ligi ndogo ya Cypriot kufuzu kucheza katika ligi kuu. Constantine
aliwahi pia kuwa mkufunzi wa mataifa ya Nepal, India, Malawi na Sudan.
Ferwafa inatarajia kukamilisha mipango hiyo
wikendi hii nchini Tunisia wakati ambapo timu ya Taifa ya Rwanda itakuwa
ikichuana na timu ya taifa ya Libya katika michuano ya kufuzu kwa mechi
za mabingwa wa Afrika zitakazochezwa 2015. Kocha msaidizi bwana Cassa
Andre Mbungo anatarajiwa kuiongoza timu hiyo wakati wa mchuano huo.
Ripoti katika wavuti wa Ferwafa zinaongezea kuwa
kuna machache ambayo wanpaswa kuzungumzwa na Constantine kabla ya
kumtangaza rasmi kama mkufunzi.
No comments:
Post a Comment