Mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya
Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 kati ya Tanzania (Serengeti Boys)
na Afrika Kusini (Amajimbos) itachezwa kwa kiingilio cha sh. 2,000.
Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam
ndiyo utakaokuwa mwenyeji wa mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 9 kamili
alasiri.
Waamuzi wa mechi hiyo wanatoka Shelisheli. Mwamuzi wa
kati ni Allister Barra wakati wasaidizi wake ni Gerard Pool na Jean Joseph
Felix Ernest wakati mezani atakuwa Nelson Emile Fred.
Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Andriamiasasoa Doda
Nirimboavonjy kutoka Madagascar.
Kikosi cha Serengeti Boys chini ya kocha Hababuu Ali
Omari kipo kambini kwa zaidi ya wiki mbili sasa kikijiandaa kwa mechi hiyo.
Mechi ya marudiano itachezwa kati ya Agosti 1 na 3 nchini Afrika Kusini.
Wakati huo huo, Alfred Kishongole Rwiza wa Tanzania
ameteuliwa kuwa Kamishna wa mechi ya marudiano ya michuano hiyo ya Afrika kwa
vijana wenye umri chini ya miaka 17 kati ya Rwanda na Uganda.
Mechi hiyo itachezwa nchini Rwanda kati ya Agosti 1 na
3 mwaka huu. Waamuzi wa mechi hiyo watatoka Burundi wakiongozwa na Pacifique
Ndabihawenimana.
No comments:
Post a Comment