Ni Brazil dhidi ya Ujerumani na Uholanzi dhidi ya Argentina katika nusu
fainali , kesho(08.07.2014) na Jumatano, lakini Brazil imedhoofika
kumkosa mshambuliaji nyota Neymar na Argentina itamkosa mchezaji muhimu
Di Maria.
Ujerumani kwa upande wake inawania kulipa kisasi dhidi ya kufungwa katika mchezo wa fainali 2002 dhidi ya Brazil.
Mlinzi Mats Hummels |
Wakati Brazil na Ujerumani zikijitayarisha kupambana katika mchezo wao
wa nusu fainali kesho Jumanne, falsafa za zamani za soka katika nchi
hizo zinaandikwa upya.
Cha kushangaza kwa mataifa hayo mawili vigogo katika kombe la dunia
zikifikia kiwango cha nusu fainali mara 24, hii itakuwa mara yao ya pili
kukutana katika kombe la dunia baada ya fainali ya mwaka 2002.
Wakati huo Ujerumani ambayo haikuwa katika kiwango cha juu kama ilivyo
hivi sasa na ambayo ilipambana tu hadi kufika fainali kwa kupata ushindi
wa bao 1-0 , wakisaidiwa na mlinda mlango wao maarufu wakati huo Oliver
Kahn , walipambana na kikosi cha Brazil kilichokuwa kimesheheni
washambuliaji hatari Ronaldo, Ronaldinho na Rivaldo.
Usiku huo mlinda mlango Oliver Kahn alifanya makosa na kukipa kikosi cha
Luiz Felipe Scolari nafasi ya kunyakua taji lake la tano la kombe la
dunia.
Scolari ndie amebakia
Hata hivyo jambo linaloweza kudokezwa tu hapa ni kwamba tangu timu hizo
kupambana miaka 12 iliyopita ni scolari pekee ambaye bado yuko
madarakani katika kikosi cha selecao Brazil na kwamba Ujerumani bado ina
mlinda mlango hodari Manuel Neuer.
Ujerumani imekamilisha pasi 500 zaidi kuliko timu yoyote nyingine katika
mashindano hayo na zaidi ya 1,000 kuliko ilivyofanya Brazil, ambayo
bado iko nyuma ya Chile licha ya kucheza mchezo mmoja zaidi.
Nusu fainali ya kesho ni mpambano wa kiakili kwa Joachim Loew , ambaye ana hatari ya kuitwa mtu aliyekaribia kupata taji.
Baada ya miaka minane akiwa kocha wa Die Mannschaft , Loew hadi sasa
ameifikisha timu hiyo katika nusu fainali moja ya kombe la dunia,
fainali ya kombe la mataifa ya Ulaya mwaka 2008 na nusu fainali ya kombe
la mataifa ya Ulaya mwaka 2012, hajaleta taji.
Ni muhimu kiasi gani kuwa watulivu katika pambano hilo kati ya Ujerumani
na Brazil , mchezaji wa kati wa Ujerumani Bastian Schweinsteiger
amesema , mchezo huo ni changamoto kubwa kabisa.
"Hata uwe na uzoefu ama umecheza michezo mingi kiasi gani, mchezo kama
huo unakuwa ni wa pekee , hususan dhidi ya wenyeji Brazil katika nchi
kama hiyo ambayo ina wazimu wa kandanda na ambayo inajitambulisha kwa
njia ya ajabu kabisa na kikosi hicho cha Selecao. Hali hiyo inaufanya
mchezo huo kuwa na hamasa kubwa. Mtu anaufurahia , anauhisi mwilini na
hupata burudani ya pekee katika mchezo kama huo."
Ujerumani itakumbana na Brazil ambayo imekuwa na mapambano ya nguvu
zaidi wakati wenyeji hao wakijaribu kunyakua taji hilo bila ya nyota wao
Neymar.
Brazil imelazimika kufanya mabadiliko bila ya mchezeshaji wa timu hiyo
Neymar pamoja na Thiago Silva ambaye hatacheza kutokana na kuwa na kadi
tatu za njano, wakati Selecao wanawania kutimiza ndoto ya kulinyakua
kombe la dunia mara sita.
Bila Neymar Brazil si chochote?
Kocha msaidizi wa Ujerumani Hansi Flick amesema jana katika mkutano na
waandishi habari kuwa kikosi chake kinafurahia changamoto hiyo.
"Ni timu ambayo ina wachezaji wa aina ya pekee, ambao wanauwezo wa
kupambana mtu kwa mtu, katika mashambulizi na hata ulinzi. Baadhi ya
nyakati hupitiliza hata mipaka iliyowekwa. Kwa hali hiyo tunatarajia
licha ya kutokuwapo Neymar na Thiago Silva , kwamba kikosi hicho
kitaweza kupata watu wa kujaza nafasi hizo na kufikia kiwango chao na
kwetu sisi tutapambana na timu imara, hicho ndio tunachokitarajia."
Kutokana na hali hiyo katika mkutano huo na waandishi habari jana
Jumapili, mchezaji wa kati wa Ujerumani Bastian Schweinsteiger amesema
mwamuzi Marco Rodriguez ni lazima aangalie sana wachezaji wa Brazil
ambao watatumia nguvu kupita kiasi katika mchezo huo wa nusu fainali
kesho na kuhakikisha faulo hazipiti bila kuadhibiwa.
Refa huyo kutoka Mexico , ambaye alikuwa mwamuzi katika mchezo ambapo
mshambuliaji wa Uruguay Luis Suarez alimng'ata mlinzi wa Italia Giorgio
Chiellini, ameteuliwa kuamua mchezo huo wa nusu fainali mjini Belo
Horizonte.
Brazil imeamua kukata rufaa dhidi ya kuzuiwa kwa Silva kucheza katika
mchezo wa kesho , lakini ni mapambano ya kutumia nguvu zaidi
yaliyoonekana sana katika mchezo huo wa robo fainali kutoka kwa wenyeji
na Schweinsteiger hataki kurejewa kwa hali hiyo.
Katika duru ya makundi timu zilizotarajiwa kusonga mbele, nyingi
zilifanya hivyo. Lakini katika awamu ya mtoano ya timu 16 , timu nyingi
zilizopigiwa upatu kutoroka na kombe hilo zilipata taabu kuvuka kikwazo
hicho. hivi sasa zimebaki timu nne.
Wabrazil wanaonekana kukata tamaa bila jogoo wao Neymar katika mchezo wa
nusu fainali dhdi ya Ujerumani pamoja na nahodha wao Thiago Silva.
Willian na Bernard , wachezaji wawili ambao wanaweza kuchukua nafasi ya
Neymar katika kikosi cha Barzil wamesisitiza jana kuwa kikosi chao
kinaweza bado kushinda taji hilo la kombe la dunia bila ya nyota huyo.
Hata hivyo Ujerumani itabidi kupambana pia na uchawi pamoja na kikosi
cha Selecao katika mchezo wa kesho wakati mtaalamu wa voodoo anapanga
kufanya vitu vyake dhidi ya Die Mannschaft.
"Nitamchukua mchezaji wao nyota na kumfunga miguu ili asiweze kukimbia
uwanjani," amesema Sillman , akimaanisha kutumia voodoo kumfunga
mwanasesere ambaye atakuwa mchezaji ambaye hakutajwa jina wa Ujerumani
hatua itakayofanyika kabla ya mchezo huo. Hivyo ni vituko kutoka huko
Brazil.
Benchi la ufundi la Uholanzi likiongozwa na Van Gaal |
Wachezaji wa Uholanzi wakipongezana |
Van Gaal akimalizia maelekezo kabla ya Jumatano kuikabili Argentina |
Argentina nayo yaikabili Uholanzi
Argentina na Uholanzi nazo zinamiadi siku ya Jumatano katika nusu
fainali ya pili ya kombe la dunia, ikiwa ni miaka 36 tangu timu hizo
zikutane katika fainali iliyokuwa na utata mwaka 1978 mjini Buenos Aires
nchini Argentina.
Kombe la dunia lililochezwa chini ya utawala wa kidikteta ulimalizika
kwa wenyeji kuwapa kipigo Uholanzi cha mabao 3-1 baada ya muda wa
nyongeza, ambapo Mario Kempes alipachika wavuni mabao 2.
Kwa Wadachi , Uholanzi , ni kipigo cha pili katika fainali, baada ya
kufungwa mabao 2-1 na Ujerumani magharibi katika fainali ya mwaka 1974,
lakini hakuna timu kutoka Ulaya ambayo imefika karibu kulinyakua kombe
hilo katika ardhi ya America kusini.
No comments:
Post a Comment