KWA MAWASILIANO ZAIDI TUMIA BARUA PEPE rockersports212@yahoo.com AU TUPIGIE KUPITIA NAMBARI 0767166607 AU 0717166607. KARIBU SANA. 66666666607 AU 0717166607

Thursday, August 28, 2014

Taarifa mbalimbali kutoka TFF: Taifa Stars sasa kucheza na Morroco, Twiga kuelekea Afrika kusini, Zoezi la usajili laongezwa kwa siku mbili

Katibu mkuu wa TFF Selestine Mwesigwa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeongeza kwa saa 48 muda wa kufanya usajili wa wachezaji kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Muda huo umeongezwa kutokana na matatizo ya mtandao yaliyojitokeza kwa siku mbili hizi (Agosti 26 na 27 mwaka huu). Awali usajili ulikuwa umalizike Agosti 27 mwaka huu, na sasa usajili utafungwa kesho (Agosti 29 mwaka huu) saa 6 usiku.
Hadi jana (Agosti 27 mwaka huu) saa 6 usiku ambao ulikuwa muda wa mwisho ni timu ya Daraja la Kwanza ya Kimondo FC ya Mbeya iliyokuwa imeingiza wachezaji wake wote kwenye system.
Kwa upande wa wachezaji kutoka nje ya Tanzania ambao wanahitaji Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) dirisha lao kwenye Mfumo wa Uhamisho wa Wachezaji (TMS) wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) litafungwa Septemba 6 mwaka huu.

TAIFA STARS SASA KUIKABILI BURUNDI
Kikosi cha Stars
Taifa Stars sasa itacheza na Burundi katika mechi ya kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) badala ya Morocco iliyokuwa icheze nayo awali kuamua kufuta mechi hiyo baada ya kushindwa kuwapata wachezaji wake wa kulipwa.
Mechi dhidi ya Burundi itachezwa Septemba 6 mwaka huu jijini Bujumbura, na kikosi cha Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kinaingia kambini Jumapili (Agosti 31 mwaka huu) mchana jijini Dar es Salaam.
Wachezaji 26 walioitwa na Kocha Mkuu Mart Nooij kwa ajili ya mechi hiyo ni makipa Deogratias Munishi (Yanga) na Mwadini Ali (Azam). Mabeki Said Morad (Azam), Oscar Joshua (Yanga), Shomari Kapombe (Azam), Nadir Haroub (Yanga), Kelvin Yondani (Yanga), Aggrey Morris (Azam), Joram Mgeveke (Simba) na Charles Edward (Yanga).
Viungo ni Erasto Nyoni (Azam), Mwinyi Kazimoto (Al Markhiya, Qatar), Amri Kiemba (Simba), Himid Mao (Azam), Salum Abubakar (Azam), Said Ndemla (Simba), Said Juma (Yanga) na Haruna Chanongo (Simba).
Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Khamis Mcha (Azam), Simon Msuva (Yanga), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC), Mbwana Samata (TP Mazembe, DRC), Mrisho Ngassa (Yanga), Mwegane Yeya (Mbeya City) na Juma Liuzio (ZESCO, Zambia).

TWIGA STARS KWENDA AFRIKA KUSINI IJUMAA

Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) inatarajia kuondoka nchini Ijumaa (Agosti 29 mwaka huu) kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya mechi ya kirafiki na timu ya Taifa ya nchi hiyo (Banyana Banyana).
Twiga Stars inakwenda huko kwa mwaliko wa Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA) kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa Jumapili (Agosti 31 mwaka huu) katika mji wa Polokwane.
Msafara wa timu hiyo utaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Saloum ambapo utajumuisha wachezaji 18 na benchi la ufundi lenye watu watano.
Wachezaji kwenye msafara huo ni Amina Bilali, Anastaz Katunzi, Asha Rashid, Donisia Minja, Esther Chabruma, Etoe Mlenzi, Fatuma Jawadu, Fatuma Makusanya, Fatuma Maonya, Fatuma Swaleh, Happiness Mwaipaja, Maimuna Said, Mwajuma Abdillahi, Mwanahamis Shurua, Shelda Mafuru, Sophia Mwasikili, Therese Yona na Zena Rashid.
Benchi la Ufundi linaongozwa na Kocha Rogasian Kaijage, na msaidizi wake Nasra Mohamed. Wengine ni Christine Luambano (daktari), Furaha Mnele (Meneja) na Mwanahamisi Nyomi (mtunza vifaa).
Timu hiyo inatarajia kurejea nchini Septemba 2 mwaka huu kwa ndege ya Fastjet.
 
KOZI YA UKUFUNZI WA UTAWALA YA FIFA KUFANYIKA DESEMBA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) wameandaa kozi ya ukufunzi wa utawala itakayofanyika Desemba mwaka huu.
Kozi hiyo itakayoendeshwa na wakufunzi kutoka FIFA itafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Desemba 1 hadi 5 mwaka huu, ambapo sifa ya chini ya elimu kwa wanaotaka kushiriki ni kidato cha nne.
Kwa wanaotaka kushiriki kozi hiyo wanatakiwa kutuma maombi yao kwa Katibu Mkuu wa TFF. Mwisho wa kupokea maombi hayo ni Septemba 5 mwaka huu ambapo wanatakiwa pia kuwasilisha nakala za vyeti vyao vya kitaaluma.

MTIHANI WA WAAMUZI, MAKAMISHNA SEPTEMBA 5
Mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness test) kwa waamuzi wanaotaka kuchezesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu huu utafanyika katika vituo viwili kuanzia Septemba 5-6 mwaka huu.
Waamuzi watakaoshiriki mtihani huo ni wenye beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na wale wa class one. Pia kutakuwa na semina wa makamishna wanaotaka kusimamia mechi za VPL na FDL ambayo itafanyika Septemba 7 mwaka huu.
Vituo vya mtihani huo ni Dar es Salaam na Shinyanga. Kituo cha Dar es Salaam ni kwa waamuzi na makamishna kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kilimanjaro, Lindi, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Njombe, Pwani, Ruvuma na Tanga.
Kituo cha Shinyanga ni kwa waamuzi na makamishna kutoka mikoa ya Arusha, Geita, Kagera, Katavi, Kigoma, Manyara, Mara, Mwanza, Rukwa, Shinyanga, Simiyu, Singida na Tabora.
Waamuzi wote ambao wamechezesha VPL na FDL msimu wa 2013/2014 na kupata matatizo au kuondolewa kwenye ligi hawahusiki na mtihani huo. Washiriki wanatakiwa kufika kituoni siku moja kabla.
Wasimamizi ni Charles Ndagala, Israel Mujuni, Issarow Chacha, Joan Minja, Pascal Chiganga, Riziki Majala, Said Nassoro, Salum Chama, Soud Abdi, Victor Mwandike na Zahara Mohamed.

MECHI ZA TIKETI ZA ELEKTRONIKI KUCHEZWA TANGA, BUKOBA
Timu za Mgambo Shooting na African Sports za Tanga zitapambana Jumapili (Agosti 31 mwaka huu) katika mechi ya majaribio ya matumizi ya tiketi za elektroniki itakayochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga kwa kiingilio cha sh. 1,000 tu.
Mechi nyingine ya tiketi za elektroniki siku hiyo itachezwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kwa kuzikutanisha timu za Kagera Sugar na Geita Gold SC ya mkoani Geita. Geita Gold iko Daraja la Kwanza.
Kabla ya mechi hizo, Ijumaa (Agosti 29 mwaka huu) saa 3 asubuhi kwenye viwanja hivyo kutakuwa na mafunzo ya matumizi ya tiketi za elektroniki pamoja na jinsi mfumo huo unavyofanya kazi.
Washiriki wa mafunzo hayo ni wasimamizi wa vituo vya Tanga na Bukoba, viongozi wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Kagera (KRFA) na Tanga (TRFA), makatibu na maofisa habari wa klabu za Kagera Sugar, Mgambo Shooting, African Sports na Geita Gold, mameneja wa viwanja vya Kaitaba na Mkwakwani na wasaidizi wao, maofisa usalama wa TRFA na KRFA, wachanaji tiketi, wasimamizi wa milangoni, wasaidizi (stewards) na waandishi wa habari.

RAIS TFF KUZURU MANYARA, KILIMANJARO, ARUSHA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atatembelea mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara.
Katika ziara hiyo atakutana na viongozi na kuangalia hali hali ya mpira wa miguu katika mikoa hiyo na mahitaji yake. Pia atazungumzia maono (vision) ya TFF katika mpira wa miguu.
Rais Malinzi atawasili mkoani Manyara, Agosti 29 mwaka huu, na ataanza ziara rasmi katika mkoa huo Agosti 30 mwaka huu. Agosti 31 mwaka huu atakuwa Arusha, na kumalizia Septemba 1 mkoani Kilimanjaro.
Katika ziara hiyo, Rais Malinzi atafuatana na Mkurugenzi Msaidizi (Wanachama) wa TFF, Eliud Mvella. Pia Septemba 8 mwaka huu, Rais Malinzi ataanza ziara ya mikoa ya Iringa, Mbeya na Njombe.

TFF YATAKA CAF IONDOE KIPENGELE AFCON
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeliandikia Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kutaka kipengele cha kutaka kwanza nchi iandae Fainali za Afrika kwa Vijana ndiyo iwe na sifa ya kuandaa Fainali za Afrika (AFCON) kiondolewe.
TFF ilishapeleka barua CAF kutaka kipengele hicho kiondolewe, na kutaka kijadiliwe katika Congress (Mkutano Mkuu) ijayo ya CAF.
Tanzania imeshaiandikia CAF barua kuomba uenyeji wa Fainali za AFCON za 2017 baada ya Libya iliyokuwa imepewe uenyeji huo kujitoa. Uamuzi wa Tanzania kuomba kuandaa fainali hizo ulifanywa na Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana Agosti 24 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment