Meneja wa klabu ya Man utd Louis van Gaal, ameahidi kuingia
sokoni na kufanya usajili wa wachezaji mara atakaporejea nchini Uingereza,
ambapo itakua ni siku chache kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi nchini
humo.
van Gaal, amesema ipo haja ya kufanya hivyo baada ya
kubaini mapungufu ya baadhi ya wachezaji wake ambao amewasoma katika kipindi
chote cha maandalizi ya msimu mpya wakiwa nchini Marekani.
Hata hivyo van Gaal, amesema pamoja na kutarajia kufanya
hivyo bado suala la nani anaondoka kikosini kwake ama anabaki, litaendelea kuwa
moyoni mwake na atalifanya kuwa siri mpaka utakapowadia wakati wa majina ya
atakaowaacha kutolewa katika vyombo vya habari.
Amesema atakachokifanya mara baada ya kurejea Old Trafford
ni kuzungumza na mchezaji mmoja baada ya mwingine na kumueleza ukweli kama yupo
katika mipango yake ama la, na katu hatofanya hivyo kupitia vyombo vya habari
ambavyo kila leo vimekua vikidadisi kwa kutaka kufahamu ni nani anaondoka ama
anasajiliwa kwenye klabu ya Man Utd.
Hata hivyo pamoja na Louis van Gaal, kuahidi kufanya
maamuzi ya kuwacha wachezaji kwa siri baada ya kufanya nao mazungumzo binafsi
atakaporejea mjini Manchester, tayari gazeti la The Mirror la nchini Uingereza
hii leo limetoka na habari za wachezaji ambao wapo kwenye wimbi la kuondoka Old
Trafford.
Wachezaji waliotajwa katika wimbi hilo kupitia gazeti la
The Mirror ni Marouane Fellaini, Luis
Nani, Shinji Kagawa, Wilfried Zaha pamoja na Anderson ambaye msimu uliopita
alipelekwa kwa mkopo kwenye klabu ya Fiorentina ya nchini Italia.
No comments:
Post a Comment