Kocha wa zamani wa Simba Patrick Liewig kuziba pengo la Vivik Nagul |
MFARANSA Patrick Liewig anatarajiwa kuchukua nafasi ya Mhindi, Vivek Nagul aliyeachia ngazi katika akademi ya Azam FC ya Dar es Salaam.
Katibu wa Azam FC, Nassor Idrissa Mohamed ‘Father’ amesema kwamba klabu hiyo imefikia makubaliano na Liewig, ambaye kwa sasa yupo Ufaransa na atakuja nchini mara moja kusaini Mkataba.
Nassor amesema klabu inatarajia makubwa kutoka kwa Mfaransa huyo aliyewahi kufanya kazi ASEC Mimosas ya Ivory Coast kwa mafanikio.
Amesema Vivek aliomba kuachia ngazi baada ya kupata kazi Chennayin FC ya Ligi Kuu ya kwao India, ambako anakwenda kuwa chini ya kocha Mkuu, Mbrazil, Zico na wachezaji maarufu kama Robert Pires, Edgar Marcelieno na Migeul Herlin.
Vivek alijiunga na Azam FC mwaka 2011 na katika kipindi hicho cha miaka mitatu na ushei, pamoja na kuzalisha vipaji vingi, pia ameiwezesha Akademi kushinda Kombe la Uhai mara mbili na Rollinstone mara moja
“Tunamtakia kila la kheri na ataendelea kuwa kwenye kumbukumbu zetu baada ya kuipa akademi mafanikio makubwa sana. Kazalisha nyota wengi ambao wamejaa timu zote za Ligi Kuu,” amesema Father.
Nassor amewataja baadhi ya wachezaji hao kuwa ni
Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wa Simba SC, Simon Msuva wa Yanga SC, wakati Azam A wapo
Manula Aishi, Gardiel Michael, Bryson Raphael, Mudathir Yahya, Kevin Friday, Farid Mussa Malik,
Joseph Kimwaga, Dizana issa na Mgaya Abdul.
KUHUSU LIEWIG;
Nassor amesema kwamba klabu imeridhishwa na falsafa ya ufundishaji ya Mfaransa huyo baada ya kumuona akifanya kazi Simba SC mwaka jana, hivyo kuamua kumchukua ahamishie mafanikio yake Chamazi.
Liewig ana Stashahada ya Juu ya ukocha na Shahada ya tatu ya ualimu wa soka ya vijana aliyotunukiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Ufaransa, Gerard Houiller na amehudhuria pia kozi za ufundishaji mazoezi ya viungo Juni mwaka 1999 katika Chuo Kikuu cha Dijon.
Kwa upande wa uzoefu, Liewig alifanya kazi PSG kuanzia mwaka 1989 hadi 1999 kama Kocha Mkuu wa akademi na kuna wakati alikuwa akishirikishwa pia katika programu za timu A, ingawa majukumu yake zaidi yalikuwa ni kwa Under 20, Under 18 aliowawezesha kutwaa Kombe la French Junior Gambardella na Under 16.
Kuanzia mwaka 1989 hadi 1990: alikuwa Meneja Mkuu wa Tomislav IVIC, 1990 hadi 1991 alikuwa Msaidizi wa Henri Michel, 1991 hadi 1994 alikuwa Msaidizi wa Artur Jorge, 1994 hadi 1996 alikuwa Msaidizi wa Luis Fernandez, 1996 hadi 1998: alikuwa Msaidizi wa Ricardo Gomez, 1998 hadi 1999 alikuwa Msaidizi wa Alain Giresse.
Liewig pia alifundisha Al Wahda FC ya Abu Dhabi kuanzia 1999 hadi 2001, ambayo aliipa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na Kombe la Ligi.
Januari mwaka 2003 alikuwa Msimamizi wa Chama cha Soka UAE katika fainali za Afrika za U20 nchini Burkina Faso.
Kuanzia mwaka 2004 hadi 2009 alikuwa Kocha wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast aliyoipa mataji matatu ya Ligi Kuu ya nchini humo mfululizo, 2004, 2005 na 2006, Super Cup ya nchini humo 2005, 2007, 2008 na 2009 na akaiwezesha kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mara tatu, mara moja akiifikisha Nusu Fainali.
Amekuwa Kocha bora wa Ivory Coast miaka mitatu mfululizo, 2004, 2005 na 2006 na tangu Septemba mwaka jana hadi Juni mwaka huu, alikuwa kocha wa Club Africain ya Tunisia.
Januari mwaka jana alitua Simba SC ambako alifanya kazi hadi mwishoni mwa msimu alipoondoka kwa sababu ya matatizo ya uongozi wa klabu hiyo.
No comments:
Post a Comment