Mshambuliaji wa zamani wa Yanga aliyehamia kwa mabingwa wa soka Tanzania Bara wana lamba lamba Azam fc Didier Kavumbagu amewachana wachezaji wa timu yake hiyo ya zamani kuwa wana tabia ya ubinafsi na kujifikiria wao wenyewe na si timu, jambo ambalo lilimfanya ashindwe kufunga magoli mengi alipokuwa na timu hiyo msimu uliopita.
Kavumbagu ambaye aliifungia Azam magoli mawili kati ya matatu katika mchezo wa ufunguzi wa pazia la ligi kuu msimu huu dhidi ya Polisi Tanzania Jumamosi iliyopita, amesema tabia ya uchoyo ilikuwa ni tatizo kwake kwasababu kila mtu alikuwa anataka kufunga goli hata kama hakuwa katika nafasi ya kufunga.
Akiongea na mtandao huu wa habari wa Rockersports, Kavumbagu bila ya kung'ata maneno amesema hilo ni tatizo sugu ndani ya kikosi cha Yanga na kwamba litaigharimu timu hiyo katika msimu huu endapo halitamalizwa.
Ingawaje hakuwa tayari kuwataja wachezaji kwa majina yao, mshambuliajia huyo raia wa Burundi alionekana kufunguka kwa kusema mchezaji anayefanya hivyo anajijua endapo atasikia habari hizi.
Msimu uliopita katika safu ya ushambuliaji ya Yanga mshambuliaji huyo alikuwa akishirikiana na Simon Msuva, Gerson Tegete, Hamisi Kiiza, Mrisho Ngasa, Saidi Bahanuzi, Hussein Javu,Haruna Niyonzima, Nizar Khalfani na Emmanuel Okwi.
Amesema anatarajia kufunga magoli mengi zaidi kuliko msimu uliopita alipokuwa na Yanga kwa kuwa kikosi cha Azam fc kinawachezaji wazuri na wanashirikiana wanapokuwa katika mwendo wa kuelekea katika goli la mpinzani.
Amewataka mashabiki wa Azam fc kuendelea kumpa sapoti kwakuwa amekwenda Azam kufanya kazi na wategemee kuona kazi yake nzuri ndani ya kikosi hicho.
No comments:
Post a Comment